KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdul-rahman Kinana amemfungulia kesi
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), kutokana na kumtuhumu
anajihusisha na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu.
Kinana
amefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutokana
na kitendo cha Mbunge huyo kutoa tuhuma hizo dhidi yake kwa nyakati
tofauti nje na ndani ya Bunge, pia alikataa kuzikanusha na kumuomba
radhi.
Inadaiwa
kuwa Aprili 21 mwaka huu Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na
Utalii alitoa tuhuma hizo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Shule ya Msingi Mbuguni wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Aidha
alizitoa bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani katika
Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka
2013/2014. Katika hati ya madai, Kinana anadai kuwa kutokana na tuhuma
hizo ameharibiwa tabia yake, uaminifu, hadhi yake kitaaluma na weledi na
kumfanya achukiwe na kudharauliwa katika jamii.
Anadai
kuwa kabla ya tuhuma hizo alikuwa katika hatua za mwisho za mchakato wa
mazungumzo ya mradi wa ubia wa kilimo cha mboga na mwekezaji kutoka
kampuni ya nje, lakini tuhuma hizo zimesababisha kampuni hiyo kuvunja
majadiliano hayo.
Kinana
anadai kuwa sababu iliyotolewa na kampuni hiyo kuvunja mazungumzo hayo
ni kutajwa kwake na mbunge huyo kuwa ni jangili anayejishughulisha na
biashara hiyo.