1.0. UTANGULIZI
Awali ya yote namshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya leo ya kuzindua Rasimu ya Katiba. pia, niwashukuru ninyi nyote mliohudhuria halfa hii ikiwa ni mwendelezo wa mchakato muhimu wa Mabadiliko ya Katiba ya nchi yetu.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilipitishwa Bungeni Novemba, 2011 na kufanyiwa mabadiliko Februari, 2012. Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu wa Kifungu 6(1) cha sheria hiyo (Cap.83). Wajumbe 34 wa Tume waliteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mwezi Aprili, 2012. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume imepewa miezi kumi na minane kukamilisha kazi yake kuanzia siku ilipoanza kazi rasmi ambayo ilikuwa Mei 2, 2012.
Tume iliandaa ratiba ya utekelezaji wa majukumu yake. Kufuatana na ratiba hiyo Tume ilijipanga kukusanya maoni ya wananchi katika kipindi cha miezi mitano kuanzia Mwezi Julai hadi Disemba, 2012. Kazi hiyo ilifanywa kama tulivyopanga. Tume ilijigawa katika makundi na ilitembelea mkoa yote thelathini.
Tume ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi wapatao 1,365,337 ambao kati ya hao wananchi 333,537 walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au kwa maandishi. Tume pia ilipata maoni ya wananchi wengi, wa ndani na nje ya nchi kwa njia mbali mbali kama vile; Mikutano ya hadhara, Fomu maalum za Tume, barua kupitia Masanduku ya Barua ya Tume, Mitandao ya Kijamii ya barua pepe; facebook ya Tume, Tovuti ya Tume; Makala mbalimbali kutoka kwenye magazeti na ujumbe mfupi wa simu.