Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na muungano wa asasi tano za kiraia uliowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia.
Kwa niaba ya mitandao hiyo mkurugenzi huyo alisema hakukuwa na haja ya kufuta matokeo hayo na kufanya maboresho kwa kuwa sababu zilizosababisha kufeli kwa wanafunzi zinajulikana na si kama serikali inavyodai kwa sasa.
Missokia alisema kabla ya serikali kutoa uamuzi huo ilitakiwa kuweka wazi mapendekezo ya Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza matokeo hayo ili wadau wa elimu wapate fursa ya kuona sababu zilizochangia kushuka kwa ufaulu katika mitihani hiyo.
“Kwa kufuta matokeo hayo bila wadau kujua sababu na kutoa mchango wao inawaaminisha Watanzania kwamba sababu nyingine hata kama zipo ziliathiri kwa kiwango kidogo matokeo hayo na suala la upangaji wa madaraja kuonekana ni sababu kubwa zaidi kuliko nyingine,” alisema Missokia.