Serikali imekubali
mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
uendelee kwa sharti la kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea
waliofika mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari leo mchana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema
uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao kati ya uongozi wa Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri Dk. Fenella Mukangara, TFF
na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Amesema baada ya
maafikiano hayo, TFF italiandikia barua Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo ndilo lililosimamisha mchakato huo ili
litume ujumbe wake kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wagombea
walioenguliwa.
Rais Tenga ambaye ameishukuru Serikali kwa kuruhusu
mchakato huo uendelee, pia ameahidi kuwa uchaguzi wa TFF utafanyika
kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali, na kuwa
haki si tu itatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali
imetuelekeza uchaguzi ufanyike kabla ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko
ni mbali. FIFA wakija hata kesho wakituambia endeleeni sisi tuko tayari.
Hesabu zetu ziko tayari, makabrasha yote yako tayari yanasubiri
mkutano tu. Labda itakuwa kutoa muda tu kwa wajumbe walioko mbali
waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi kuwaita ghafla,” amesema.
Amesisitiza kuwa TFF
ilishapanga tarehe ya uchaguzi, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya
baadhi ya walioenguliwa kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki
uchaguzi kwa sababu wanataka kuendelea kubaki madarakani haya maana
hata kidogo.
Hivyo amewataka wagombea wote waliofika kwenye
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wakaendelea kujiandaa vizuri, kwani
FIFA watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
Pia amesema TFF ina
heshimu Serikali na itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima
iheshimu FIFA sababu iko kwenye mpira wa miguu, na FIFA ndiyo
wasimamizi wa mchezo huo duniani.
Amewakumbusha
wanachama wa TFF, hasa wajumbe wa Mkutano Mkuu kufahamu kuwa TFF ina
katiba, lakini ni lazima pia wafahamu kwanini kuna FIFA.
Rais Tenga
amewahadharisha watu wanaopitapita mikoani kuomba saini za wajumbe ili
kuita Mkutano Mkuu wa dharura wakati wanajua mkutano ulishaitishwa,
lakini ukasimamishwa na FIFA. Jambo hilo kikatiba ni kosa.