Kwa nini tukae siku 87 au 90 wakati tunajua upande wa pili
haujakamilika? Kwa mujibu wa sheria inatakiwa ridhaa ya theluthi mbili.
Mwigulu Nchemba
Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kimeanza kumeguka baada ya baadhi ya wabunge wake ambao
ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuunga mkono kauli ya Naibu
Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba.
Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,
Jumanne iliyopita akichangia wakati wa mjadala wa mabadiliko ya kanuni,
alilitaka Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima wa
kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili.
Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84
bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili
inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya, hakiwezi kueleweka kwa
Watanzania.
Nchemba alisema ni vyema kujua idadi ya
wanaoshiriki awamu ya pili ya Bunge hilo ili kutoa uthibitisho
kimahesabu kama uamuzi wa kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.
Jana Mwigulu Nchemba alizidi kusisitiza kauli
aliyoitoa akisema ni msimamo wake binafsi kama mtoto wa maskini. Alisema
anatambua jinsi walipa kodi watakavyoumia, rasimu hiyo itakapokwama
kupita kutokana na kukosekana kwa theluthi mbili ya pande zote.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye juzi alijibu akisema kauli ya Nchemba ni mtazamo wake
binafsi na hakuongea kama kiongozi wa chama hicho.
Lakini jana wabunge mbalimbali wa CCM walijitokeza
hadharani wakisema wanaunga mkono kauli ya Nchemba ili hesabu ijulikane
badala ya kuendelea kutafuna fedha za wananchi bila tija.
Ali Keissy
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy, alisema
msimamo wa Nchemba ndiyo msimamo sahihi ambao unapaswa kufuatwa kuliko
kuendelea na Bunge wakati wakijua kuwa theluthi mbili haitapatikana.
“Kama kuna wabunge wa CCM wanaounga mkono kauli ya
Mwigulu kwa asilimia 100 basi mimi naunga mkono kwa asilimia 500 na
wako wabunge wengi tu wa CCM wanaunga mkono,” alisema. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz