Bi. Mary Nsemwa mwezeshaji TGNP mtandao
Waandishi wa habari wamehimizwa kuandika habari za kijamii zinazowahusu wananchi moja kwa moja ili kuwasaidia wananchi kupaza sauti na kuepuka habari za kichochezi.
Mwezeshaji wa warsha ya mafunzo kwa waandishi wa habari mkoa wa Mbeya Bi. Mary Nsemwa ameyasema hayo katika warsha iliyofanyika jana katika ukumbi wa Coffee Garden jijini Mbeya.
"Ukiandika habari zinazolenga maisha ya watu wa hali ya chini na kuibua kero zao huko vijijini hautaitwa mchochezi na ukizingatia Mh. amejipambanua kuwa yeye ni mtu wa watu maskini na ana nia ya kuwainua anaweza kufanya lolote katika kuwasaidia" alisema Bi. Nsemwa.
Aidha Nsemwa ameongeza kuwa vyombo vya habari ni kiungo muhimu kati ya wananchi waishio vijijini wasioweza kupaza sauti kuwafikia viongozi wa ngazi za juu kuwaeleza kuhusu changamoto zinazowakabili.
"Waandishi wafuateni wananchi vijijini, wana kero nyingi zinazowakabili ila hawawezi kupaza sauti, nyie ndio mnaweza kuwa msaada wa kuzifikisha shida zao kwa viongozi wa juu" alisema Bi. Nsemwa.
Wakichangia hoja katika warsha hiyo baadhi ya waandishi wa habari walieleza changamoto zinazowakumba wakati wa kuchakata habari za kijinsia kuwa ni pamoja na uhaba wa raslimali fedha, vitendea kazi, na vitisho toka kwa baadhi ya wanajamii wakati wakitekeleza majukumu yao.
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni taasisi huru inayotoa chachu ya ujenzi wa tapo la harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi nchini Tanzania, barani Afrika na kwingineko duniani.
No comments:
Post a Comment