Friday, March 09, 2018

KENYATTA, ODINGA WAKUTANA IKULU, WAKUBALIANA JAMBO

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo Raila Odinga katika ofisi yake Jumba la Harambee, Nairobi.

Mkutano huo umefanyika muda mfupi kabla ya Bw Kenyatta kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson.

Marekani imekuwa ikihimiza kufanyika kwa mazungumzo na mashauriano kutatua mzozo wa kisiasa uliokumba taifa hilo baada ya uchaguzi uliojaa utata mwaka jana.


Bw Odinga alitangulia kuhutubia taifa moja kwa moja na baadaye Bw Kenyatta akatoa hotuba yake.

Bw Kenyatta amesema wamekubaliana na Bw Odinga kwamba taifa la Kenya ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.

Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na uchaguzi ujao bali "uthabiti wa taifa."

"Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya wananchi lazima iongoze."

"Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna araia anayehisi ametengwa."

"Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu."

"Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa tumeungana kama Wakenya."

Bw Odinga amesema kwa muda mrefu Kenya imeangazia kubadilisha taasisi na miaka saba iliyopita katiba mpya ilianza kutekelezwa.

"Sasa lazima tuwe na ujasiri wa kukubali kwamba hilo halijafanikiwa. Bado hatujabadilisha mengine," amesema Bw Odinga.

"Ndugu yangu na mimi tumekutana pamoja leo na kusema yamefikia kikomo. Tumekataa kuwa watu ambao chini yake Kenya imekuwa taifa lililofeli."

Amesema wamekubaliana kufanikisha mabadiliko yatakayofanikiwa mageuzi nchini humo, na pia kukomesha kulaumiana.

Amewataka Wakenya waunge mkono mpango wa viongozi hao wawili.

"Tumesafiri mbali sana kiasi kwamba hatuwezi kurudi tena bandarini. Isitoshe, hatuwezi kufika tunakoenda bila kufanya mabadiliko la sivyo tutazama baharini," amesema Bw Odinga.

"Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja. Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha hapa na sisi. Tutembee pamoja," amesema Bw Odinga.

Chanzo BBC Swahili. 

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...