Friday, January 08, 2016

WAZIRI ACHUKIZWA NA MADARAJA YA UFAULU

VITA ya kupambana na utendaji kazi usiokuwa na tija kwa Taifa kwa watendaji wengi wa taasisi za Serikali imezidi kushika kasi baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kumtaka Katibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde kumwandikia maelezo ya kitaalamu yaliyosababisha kubadilishwa kwa mfumo wa upangaji viwango vya ufaulu kutoka wa madaraja (Division) hadi wastani wa pointi (GPA).

Pia amemtaka kumweleza sababu zilizowafanya kuongeza mtihani (Continuous Assesment) kwa wanafunzi wa kujitegemea ili ajiridhishe pamoja na viongozi wengine wa wizara iwapo mabadiliko hayo yana tija kwa Taifa au la.

Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha menejimenti ya baraza hilo.


Alisema agizo hilo linapaswa kutekelezwa ndani ya siku saba kuanzia jana kwa kuwa mfumo huo haueleweki.

Profesa Ndalichako alisema mojawapo ya maeneo ambayo yanampa maswali mengi bila majibu ni kwenye viwango vya ufaulu na upangaji wa madaraja.

“Jana nilikutana na wamiliki wa shule binafsi wakahoji juu ya mfumo huu, hata nilipoondoka kwenye nafasi ya Katibu Mtendaji wa NECTA, bado nilikuwa napokea maswali mengi kutoka kwa wananchi waliokuwa na namba zangu,” alisema.

Alisema wananchi hao wamekuwa wakimtaka awafafanulie juu ya tofauti ya mifumo hiyo na faida zake.

“Wakati nikiwa katibu, mojawapo ya mambo ambayo nilikuwa nikiyakataa ni haya, kwa sababu kunapokuwa na viwango tofauti kunasababisha mkanganyiko… mnasema wa awali ulikuwa na malalamiko, mbona sikuwahi kuyapokea?

“Kwa maana hiyo, nataka mnieleze kwanini ninyi mlihama kutoka ‘division’ hadi GPA, mfumo huo una faida gani na kabla ya kuupitisha mlijadiliana na wadau gani,” alisema.

Waziri huyo ambaye alilitumikia baraza hilo katika nafasi hiyo ya katibu mtendaji kwa muda wa miaka tisa, alisema mojawapo ya taasisi ambazo atazinyima usingizi ni NECTA, kwani ni muhimu katika kupima kiwango cha elimu nchini.

Alisema atahakikisha anaendeleza kasi ya utendaji kazi aliyokuwa nayo hapo awali, lakini kwa nafasi yake aliyonayo sasa atafuatilia sekta ya elimu kwa ukaribu maeneo yote.

“Nataka NECTA mfanye kazi kwa weledi, kwa kusimamia misingi mizuri ya kimaamuzi tuliyokuwa tumejijengea kuendesha shughuli, msifanye uamuzi usiokuwa na tija.

“Lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuinua kiwango cha ubora wa elimu, mnapaswa kupanga viwango vya ufaulu kwa kitaalamu, changamoto ya vijana kuhitimu elimu yao wakiwa hawajui chochote ni shida, na ili tuseme mtu amesoma lazima tumpime kwa kiwango chake cha uelewa, anaweza kufanya nini,” alisema.

Alisema jambo jingine ambalo atalifuatilia kwa ukaribu ni michanganuo ya ufaulu kwani ndiyo itakayowapa dira na kupima kiwango cha ubora wa elimu wanayopatiwa wanafunzi.

“Nilipokuwa hapa, wakati mwingine nilikuwa naishiwa hadi hamu ya kula wakati wa kutangaza matokeo kwa sababu unakuta shule nyingine wote wamepata daraja F, sasa katika hali kama hii lazima kuna tatizo, haiwezekani wote wafeli, kuna jambo la msingi la kufuatilia,” alisema.

Kwa upande wake, Dk. Msonde alisema mabadiliko hayo yalifanyika baada ya baraza kupokea maelekezo ya kisera kutoka wizarani.

Alisema wizara ilisema mfumo huo ungekuwa na faida hapo baadaye na utaunganishwa kwenye mfumo wa Serikali mtandao (E-Government).

“Kwa kuzingatia hilo, tulibadilisha ili kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye ngazi ya elimu ya juu, kukabili vyeti bandia pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii kwa sababu kulikuwa na maswali, kwanini mwenye alama nyingi anafeli, lakini mwenye ndogo anaendelea,” alisema.

Kuhusu hoja ya kufanikisha udahili wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya juu, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia elimu ya juu, Profesa Simon Msanjila, alisema si sahihi kwani huwa hawatumii GPA zaidi ya kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi husika kwa mfumo wa madaraja..

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...