Wednesday, November 25, 2015

BARAZA LA MAWAZIRI LABADILISHWA...!!!


Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya amefanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri, na kuwaacha wote wizara zao zilizotajwa katika ufisadi. 

Rais Uhuru Kenyatta amechukua hatua hiyo siku moja tu baada ya kutangaza ufisadi kuwa tishio kwa usalama wa kitaifa.

Rais ameahidi kufanya mabadiliko zaidi katika afisi yake hivi karibuni. Katika hotuba ilioonyeshwa kwa njia ya Televisheni, Rais Uhuru Kenyatta ameongeza idadi ya wizara kutoka kumi na tisa hadi ishirini na kuongeza idara mpya chini ya wizara mbalimbali katika kile alichosema ni kusaidia mawaziri kutekeleza majukumu yao bora zaidi .


 Idara hizo zimeongezwa kutoka ishirini na sita hadi arobaini na moja.

Rais Kenyatta amefanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri baada ya mawaziri sita kulazimika kujiondoa kutokana na wizara walizosimamia kuhusishwa na ufisadi huku wawili kati yao wakikabiliwa na kesi mahakamani.

Ni Mabadiliko yaliyotarajiwa hasa baada ya hatua ya aliyekuwa waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru kujihuzulu mwishoni mwa juma kutokana na kile alichosema ni ushauri wa daktari wake- baada ya usumbufu aliopata wizara yake ilipohusishwa na sakata kadhaa za ufisadi.

Kwa mujibu wa katiba idadi ya mawaziri inapaswa kuwa kati ya kumi na wanne na ishirini na wawili- na hivyo kujiuzulu kwake kulisababisha idadi hiyo kupungua hadi kumi na tatu.

Baraza jipya la mawaziri linajumuisha wanawake wanne na wanaume kumi na sita.

Baadhi ya mawaziri wamesalia katika nafasi zao huku wengine wapya wakiteuliwa kuchukua nafasi za mawaziri waliohusishwa na ufisadi.

Hatua itakayofuata sasa ni kwa mawaziri wapya kuchunguzwa na kamati ya bunge kabla ya kuidhinishwa kikamilifu.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikikabiliwa na changamo ya ufisadi katika wizara kadhaa na kumekuwepo shinikizo sio tu kutoka kwa wananchi lakini pia kutoka kwa mashirika ya kijamii,viongozi wa upinzani na hata mabalozi wa nchi za kigeni kutaka hatua zichukuliwe.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...