Wednesday, June 24, 2015

WAZIRI GHASIA, KAFULILA WATOFAUTIANA BUNGENI

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila 

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia jana walitofautiana bungeni kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha zinazomkabili Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.

Tukio hilo lilitokea baada ya swali la nyongeza la mbunge huyo, aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu Nyembo aliyedai kutoa kauli ya kutaka Wabembe waende kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyosababaisha Wabembe kukamatwa na kupelekwa ubalozini, ambapo ubalozi wa DRC , uliwakataa na kusababisha wanyanyasike kwa karibu wiki mbili. 

Pia Mbunge huyo alidai Mkuu huyo wa Wilaya aliondolewa wilayani Chato akihusishwa na ufisadi wa mbolea yenye thamani ya Sh bilioni 1.5 na kwamba sasa ana kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Chato, hivyo serikali haioni aibu kuwa na Mkuu wa Wilaya wa aina hiyo, ambaye anashitakiwa na serikali yenyewe.

Akijibu swali hilo, Waziri Ghasia alisema ingekuwa vigumu kwa serikali kutoa tamko kwa jambo hilo, kwani haina uhakika kama kweli kauli hiyo ndiyo iliyosababisha matatizo ya watu kukamatwa. 

“Hatuwezi kutoa kauli kwa sababu uhakika kwamba kauli ya Mkuu wa Wilaya ndiyo iliyosababisha watu wengine kukamatwa, hilo hatuna uhakika nalo.

“Kuhusu Mkuu wa Wilaya kuwa na kesi mahakamani bado ni tuhuma, na wizi wa mbolea anayosema Mheshimiwa Kafulila, mimi mwenyewe nilifutilia hiyo kesi na anatuhumiwa kuiba Sh 250,000, nilichukua hatua, niliandika barua ofisi zinazohusika kupata uhakika, biashara ya zaidi ya Sh milioni 300 zipotee Sh 250,000 mpaka leo sijapata majibu.

“Ikumbukwe tuhuma ni tuhuma, ni Mahakama pekee ndiyo itakayoamua kama kweli ana kosa au la, kama kuna matatizo mengine jimboni namuomba Mheshimiwa Kafulila ajiandae na uchaguzi unaokuja,” alisema Waziri Ghasia.

Katika swali lake la msingi, Kafulila alihoji nini msimamo wa serikali kuhusu kauli ya Nyembo aliyoitoa wakati akihutubia Kijiji cha Karago, Uvinza ambapo alisema wabembe wote wanatakiwa warudi DRC.

Hivyo mbunge huyo alitaka kauli ya serikali juu ya hatima ya uraia wa jamii za wabembe ambao alisema ni zaidi ya robo ya wakazi wa Wilaya ya Uvinza.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...