Friday, March 27, 2015

GWAJIMA ASAKWA NA POLISI KWA KUMKASHIFU KARDINALI PENGO

GWAJIMA
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemtaka Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kujisalimisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.


Hatua hiyo ya polisi imekuja baada ya jeshi hilo kupokea malalamiko, ambapo inadaiwa Mchungaji Gwajima alitoa lugha ya kashfa dhidi ya Kardinali Pengo ambaye alipinga tamko lililotolewa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) la kuipigia kura ya Hapana Katiba Inayopendekezwa.


Taarifa iliyotolewa jana na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi, Kamishna Suleiman Kova, imemtaka Mchungaji Gwajima kujisalimisha haraka katika Kituo cha Polisi cha Kati kwenye Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kashfa na matusi.

Kova alisema jeshi hilo limepokea malalamiko ya kukashifiwa na kutukanwa hadharani Kardinali Pengo.

Alisema matusi hayo yameonekana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya WhatsApp na mingineyo, ambapo kuna sauti iliyorekodiwa na picha za video zikimuonyesha Mchungaji Gwajima akimkashifu na kumtukana kwa maneno makali Kardinali Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.

Kova alisema baada ya tukio hilo, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kumpata Mchungaji Gwajima bila mafanikio.

“Ni muhimu sana kwa Mchungaji Josephat Gwajima aripoti mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii.
  “Jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri hili unaendelea ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Kova.
 VIDEO YA GWAJIMA
Hivi karibuni sauti iliyorekodiwa na picha za video zilionekana katika mitandao ya kijamii ambazo zilikuwa zikimtukana Kardinali Pengo.

Sehemu ya maneno hayo ambayo yanamwonyesha Gwajima akizungumza kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp na Facebook ni; “Pengo unaaibisha kama mtoto mdogo aliyevaa pampasi aliyebebwa na mama yake, Pengo ni mjinga asiyefaa, juzi aliokoka kwa kula chakula chake ovyo ovyo, sijui kala maharage ya wapi?


“Pengo awe Mkatoliki amejishushia heshima yake mwenyewe, aache uaskofu awe mkulima wa kawaida, hafai mzee ametudhalilisha kabisa na amewageuka maaskofu wote kwa kile walichopatana .
Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz. 


“Amewadhalilisha maaskofu wote, amedhalilisha CCT, amedhalilisha CPCT, pia amewadhalilisha Watanzania wote.”

GWAJIMA NI NANI
Gwajima ni mwasisi na mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ambapo kwa sasa anaongoza waumini wapatao 70,000 kwa siku, na hivi sasa yuko mbioni kuanzisha makanisa mengine mikoa yote ya Tanzania.

Kwa mujibu wa kauli zake alizopata kuzisema huko nyuma katika moja ya mahubiri yake kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe jijini Dar es Salaam, hivi sasa ana waumini wengi kuliko makanisa mengine kutokana na huduma nzuri anayotoa kwa waumini na jamii kwa jumla.


“Nimefanikiwa kuwa na waumini wengi kuliko wengine kwa sababu nahubiri Neno tu, sirushiani maneno na makanisa mengine.
“Sisi hatuna utamaduni wa kuwashambulia wachungaji wenzetu. Wao hata wakitusema vipi, sisi tunakaa kimya kwani kujibishana kunaleta mgawanyiko.”


GWAJIMA NA FLORA MBASHA
Februari 4, mwaka huu picha za mtoto mchanga zilisambazwa katika mitandao ya kijamii na kudaiwa kuwa ni wa mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Flora Mbasha aliyezaa na Mchungaji Gwajima.

Hatua hiyo ilikuja miezi kadhaa tangu Flora aingie katika mgogoro wa ndoa na mumewe Emmanuel Mbasha aliyefikishwa mahakamani kwa kosa la ubakaji.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu taarifa za picha za mtoto huyo, Mchungaji Gwajima alisema ni za uzushi na huenda zinasambazwa na mume wa Flora, Emmanuel Mbasha.


Mchungaji Gwajima alikwenda mbali na kusema pamoja na uzushi huo unaosambazwa dhidi yake kwa kuhusishwa katika uhusiano na Flora, anamwachia Mungu kila kitu.

“Si unajua hiyo issue (suala, jambo) ya Mbasha ni ya muda mrefu tu… wakati mwingine mimi huwa sijibu ujinga.

“Awali niliwaza kuwashtaki (alipoanza kuhusishwa kwamba ana uhusiano na Flora) wanaoeneza uzushi huo, lakini nikaona ‘It doesn’t hold water’ (haina mashiko), najua shutuma hizo zinatoka wapi,” alisema Mchungaji Gwajima.
Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...