Saturday, November 15, 2014

BUTIKU AMKINGIA KIFUA WARIOBA

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Mwalimu Nyerere , Joseph Butiku 

Taasisi ya Mwalimu Nyerere imesema kuwa wanaotaka aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akae kimya kuhusu Katiba Inayopendekezwa hawana hoja.
Imesema kuwa wanaosema hivyo hasa wale wa chama tawala (CCM) wanatakiwa kujiuliza kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita wamefanya nini kuhusu Katiba, ikisisitiza kuwa itaendelea kufanya midahalo ya kuwaelimisha Watanzania kuhusu mchakato wa Katiba ili utakapofika wakati wa kura ya maoni waelewe kipi wanatakiwa kukifanya kwa mustakabali wa taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Joseph Butiku alisema hayo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu kazi na majukumu ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere tangu ilipoanzishwa hadi sasa. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Butiku alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kufanya utafiti utakaochangia kutatua matatizo mbalimbali kwa njia ya mazungumzo na amani kama ambavyo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyokuwa akiamini.
Kauli hiyo ya Butiku inakuja siku chache baada ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kukaririwa akisema: “Kadri anavyoendelea kupiga kelele, Jaji Warioba sasa anatutia wasiwasi kwamba, yale siyo maoni ya wananchi, bali ni maoni yake. Ndiyo maana anayatetea.”
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo alisema: “Sisi tuna nia njema, Mzee Warioba anataka kuangamiza nchi hii kwa matakwa yake.”
Kwa upande wake Mbunge wa Mbinga (CCM), John Komba alisema: “Jaji Warioba ni Shida kutokana na kuendelea kujihusisha na mchakato huo.”
Pia, Butiku jana alisema: “Tunachokifanya sasa siyo kuwashawishi Watanzania kukataa au kukubali Katiba Inayopendekezwa bali kuwaelimisha ili wafahamu kilichomo ndani ya Katiba hiyo, hivyo sisi sote ni washiriki kama wengine.”
Alisema kuwa midahalo kama ya elimu, uchumi na siasa imefanyika na sasa Watazania wanasema tunataka ifanyike midahalo inayohusu Katiba kwa lengo la kujibu maswali na siyo kuwaacha njiapanda.
Akizungumza kwa hisia Butiku ambaye ni kada wa CCM alisema: “Hili jambo ni la Watazania, hakuna mtu anayetakiwa kutetea hoja zake. Tunazungumza kuhusu mustakabali wa taifa, hivyo tusianze kubaguana kama mtu alikuwapo au hakuwapo si hoja: Kama ni hivyo, watu wa CCM walikuwapo miaka 50, wamefanya nini kuhusu Katiba?”
Aliongeza: “Kama hoja ni kuwa na Katiba Mpya na hii iliyopo mnaitukuza na kusema hili na lile, Warioba hana kosa kuendelea kushiriki katika mchakato huu na anashiriki kama raia mwingine au mshiriki mwingine. Tuwaache Watanzania wawe huru, wasitishwe na mtu yeyote, wasihongwe na wawe huru kutengeneza Katiba yao.”
Alikifafanua alisema: “Sasa hivi watu wote wa Serikali, Rais, Makamu wa Rais, mawaziri au mtu yeyote ni washiriki tu katika mchakato huu, kwani Watanzania bado hawajamkabidhi kiongozi wao Katiba. Nchi hii ni huru, hivyo tuepuke kuuharibu mchakato huu. Vijana acheni kuwa makuwadi wa kuhongwa, huo ni uhuni ambao vijana wanatakiwa kuuepuka.”
Mdahalo
Kuhusu mdahalo uliotakiwa kufanyika kesho alisema kuwa umeahirishwa hadi baadaye ili kuweka mambo sawa kwa kuongeza watoa mada na washiriki wa kada mbalimbali kujitokeza kufafanya Katiba Inayopendekezwa.
“Katiba siyo ya kundi lolote…Tunataka kuhubiri hicho kwa njia ya amani, Katiba haiweze kutengenezwa na Ukawa pekee yao, Katiba haiwezi kutengenezwa na CCM pekee yao au ikatengenezwa na madaktari pekee, bali Katiba inatengenezwa na Watanzania wote.”
“Mimi sasa sio mjumbe wa tume, Warioba siyo mjumbe wa tume, Rais (Jakaya Kikwete) siyo mjumbe wa tume, mbona walikusanyana pale Dodoma na kushangilia na kutengeneza utaratibu wa kusema ni nzuri ni nzuri.”
“Sikiliza mbunge wako, sikiliza rais wako, sikiliza waziri wako, sikiliza Warioba na sikiliza aliyeaminiwa sasa hivi wote, kwani sasa hivi watu wote ni wachangiaji tu. Tusiseme kuwa ulikuwa mjumbe wa tume au mjumbe wa Bunge la Katiba usichangie si kweli,” alisema Butiku.
Aliongeza: “Nenda kwa Chenge au njoo kwangu nitakueleza…Utakuwa mtu wa ajabu kama utashindwa kwenda kwa Warioba au utampinga eti kwa kuwa alikuwa mwenyekiti wa tume, wewe unajua kila kitu kilichoandikwa humo, unajua historia yake, wao wanajua, mbona tumewaleta watu kutoka nje na hamuulizi…Mbona Bunge limeleta watu kutoka nje.”
“Vyama viache Watanzania watengeneze Katiba yao, Serikali iache Watanzania watengeneze Katiba yao, sisi wote tuwasaidie Watanzania kutengeneza Katiba yao,” alisema Butiku.
Butiku alisema: “Tusiwalazimishe, tusiwatishe, tusiwahonge, kwa nini tuwahonge vijana kutengeneza Katiba yao?...Tuwaache Watanzania watengeneze Katiba iliyo bora kwa manufaa ya taifa lao.”
Akizungumza kwa upole huku akitumia vitabu mbalimbali ikiwamo Katiba ya CCM na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 alisema vyama vya siasa hususan vikubwa ndivyo vinavuruga mchakato huu.
Alisema kitendo cha vyama kuhodhi mchakato huo kilianza wakati Tume ya Katiba ilipowasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba kwa kila upande kuvutia kwake jambo ambalo limesababisha mchakato huo kufika hapa. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...