Saturday, October 11, 2014

MAOFISA POLISI 120 WATIMULIWA CCP

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu  

Moshi. Maofisa wa Polisi wapatao 120 wa Jeshi la Polisi, waliokuwa wakihudhuria mafunzo ya kupandishwa vyeo katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wametimuliwa chuoni hapo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana kutoka ndani ya chuo hicho zamani kikijulikana kama CCP, zimedai uamuzi wa kuwaondoa chuoni ulitangazwa jana na mkuu wa chuo hicho, Matanga Mbushi.
Vyanzo mbalimbali vililidokeza gazeti hili kuwa, waliotimuliwa chuoni hapo ni maofisa ambao wana ulemavu wa aina mbalimbali walioupata wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi.
Habari hizo zilisema hadi jana saa 9:00 alasiri, maofisa hao walikuwa ofisi za mkuu wa chuo hicho wakisubiri kupatiwa maelekezo ya namna ya kurejea katika vituo vyao vya kazi mikoa mbalimbali. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Wako 120 hivi walikuja hapa (MPA) kwa ajili ya kuchukua kozi za Koplo, Sajenti, Meja na ‘Assistant Inspector’ (wakaguzi wasaidizi), lakini ndiyo hivyo wametuambia tuondoke,” kilidokeza chanzo chetu.
Hata hivyo, ofisa mmoja alilidokeza gazeti hili kwamba mkuu wa zamani Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ambaye amestaafu, ndiye wa kulaumiwa kwa kutoheshimu mapendekezo ya wataalamu.
“Tulimwambia IGP Mwema kwamba ni vizuri kama maofisa wenye ulemavu kama baadhi ya vigezo wanavyo basi wapewe vyeo huko huko mikoani, lakini wasiende chuoni,” alidokeza na kuongeza;
“Tulipendekeza yafunguliwe madarasa ya kanda wakishafanya mtihani wa kawaida wapewe vyeo huko huko, lakini wakija chuoni ni lazima wahudhurie vipindi vyote ambavyo vinafanya chuo kiitwe chuo.
“Chuo chochote kile kina vigezo vyake na kwamba ili mtu apate cheo alichokwenda kukisomea ni lazima ahudhurie asimilia 95 ya vipindi ikiwamo kwata, medani za kivita na kuzuia vurugu,”alisema.
Chanzo kingine kililidokeza gazeti hili kuwa maofisa hao waliripoti chuoni hapo wiki mbili zilizopita na katika uchunguzi, walibainika wana ulemavu ambao hawawezi kumudu mafunzo ya ukakamavu.
Mmoja wa maofisa hao waliotimuliwa alilalamika kuwa kitendo hicho siyo cha kiungwana kwa kuwa ulemavu huo waliupata wakiwa kazini wakilitumikia Taifa na hawajashindwa kuingia darasani.
“Baadhi yetu tumefanya kazi miaka 20 wengine 25. Wamekatika miguu. Wako trafiki wamegongwa na polisi wengine wamepigwa risasi na majambazi wakapata ulemavu si sawa kutunyima vyeo,” alidai.

Ofisa huyo alisema pamoja na ulemavu huo, lakini wamekuwa wakipangiwa kazi na kuzimudu kama kawaida isipokuwa zile za ukakamavu na kwamba hata wakati wakipendekezwa, walikuwa wanajulikana matatizo yao.
Alipoulizwa na gazeti hili jana, Mbushi alithibitisha kuwapo kwa uamuzi wa kuwaondoa chuoni maofisa hao, lakini akasema wanasubiri maelekezo zaidi kutoka makao makuu ya polisi.
“Bado hatujawaondoa lakini ukweli ni kwamba kama mtu hawezi kumudu mafunzo lazima aondolewe. Kama mtu hawezi kuingia kwenye paredi anakosa vigezo vya chuo,” alisema na kuongeza;
“Tunawasiliana na makao makuu ili tuone wataamua nini, lakini kwa kweli hawawezi kumudu mafunzo ni wagonjwa wameumia, wengine miguu mibovu na mafunzo ni ya kijeshi siyo darasani pekee,” alisema na kuongeza:
“Ni lazima tuchukue kila aina ya tahadhari unaweza kulazimisha halafu mtu akafa kwa sababu mafunzo hasa ya ujasiri ni magumu, lakini kumbe mtu amekuja ni mgonjwa,” alisisitiza Mbushi na kuongeza;
“Kwa hiyo wamependekezwa kupata vyeo kwa utaratibu wa kawaida kabisa ndani ya Jeshi la Polisi wanaingia darasani kama kawaida, lakini gwaride ambalo ni sehemu ya mafunzo hawawezi.” Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...