Kamati Kuu ya Chadema imeazimia
kuendesha kampeni ya kupinga Katiba Inayopendekezwa kwa viongozi wake
wakuu pamoja na wale wa mabaraza yake kufanya ziara katika mikoa
mbalimbali nchini.
Hatua hiyo imekuja siku tatu, tangu Rais Kikwete
autangazie umma wa Watanzania alipokuwa akihutubia kilele cha Mbio za
Mwenge mkoani Tabora kwamba Katiba Inayopendekezwa inafaa hivyo kuwataka
Watanzania waipigie kura wakati wa mchakato wa kura ya maoni.
Ziara ya Chadema itaanzia katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa ambako itachukua siku 20 ikiongozwa na Baraza la Wanawake
(Bawacha), linaloongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na baada ya
kumaliza, itaanza ziara nyingine ya siku 20 itakayofanywa na Baraza la
Vijana (Bavicha).
Dk Slaa alisema CCM wameanza kazi ya kuwataka
wananchi kupiga kura ya ‘ndiyo’ na Chadema wanaanza mikutano ya
kuwashawishi wananchi kuikataa kwa kuipigia kura ya ‘hapana’.
Alisema kuanzia Novemba 5 mwaka huu, viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho nao wataanza ziara katika mikoa mbalimbali nchini.
“Bawacha ndiyo itakuwa timu ya kwanza. Itakwenda
Mwanza mjini, Ukerewe, Magu, Sengerema, Geita, Busanda, Bukombe,
Biharamulo, Muleba, Karagwe, Bukoba Mjini, Chato, Shinyanga Mjini na
Maswa Mashariki,” alisema Dk Slaa. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alisema uchakachuaji uliofanyika katika Bunge la
Katiba umezaa Katiba isiyotokana na maoni ya wananchi, kwamba kazi
iliyopo sasa ni kuipigia kura ya ‘hapana’ kwa sababu inabeba kundi
fulani la watu wachache.
“Itakayopatikana si Katiba ya Tanzania ni Katiba
ya CCM. Chama hiki kiliandaa rasimu yake na kuhakikisha kuwa inaingizwa
katika Katiba Inayopendekezwa. Mwaka 2011 Halmashauri Kuu ya CCM (Nec)
iliagiza viongozi wa CCM kuhakikisha kuwa mambo yote yanayopigiwa debe
na chama hicho yaingizwe katika Katiba na hilo limefanikiwa,” alisema na
kuongeza:
“Tunapenda kuwaeleza Watanzania, asasi mbalimbali
na taasisi za dini kuwa wakati umefika. Sasa tuache kulialia, kulalamika
na kunung’unika.”
Tafsiri ya Katiba
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alieleza
hatua mbalimbali zinazotoa tafsiri ya wazi jinsi Katiba Inayopendekezwa
inavyokosa uhalali wa kupigiwa kura ya ‘ndiyo’ katika kura ya maoni.
“Kwanza Bunge Maalumu la Katiba lilijigeuza Tume
ya Katiba na kuanza kukusanya upya maoni ya makundi mbalimbali. Wajumbe
waliokuwa nje ya Bunge hilo kuruhusiwa kupiga kura na wale waliopiga
baadhi ya Ibara kuhesabiwa kuwa wamepiga kura ya ‘ndiyo’,” alisema
Lissu.
Alisema hata baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walioelezwa kuwa
wangepiga kura katika balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali,
haijaelezwa walipigia kura hizo wapi.
“Wajumbe wa Bunge la Katiba, Mohamed Raza na Salim
Turky wote kutoka Zanzibar waliharibu kura zao, lakini zilizoharibika
zilihesabiwa kura halali.
Hata hivyo Raza na Turky walipotafutwa jana kupitia simu zao za mkononi kuzungumzia suala hilo hawakupatikana. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alisema hata wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kutoka Zanzibar na wengine waliosusia vikao vya Bunge
hilo na ambao hawajulikani majina yao hadi sasa, zilihesabiwa kura
halali za ‘ndiyo’.
“Maulida Komu alikuwa Ukawa, katika Gazeti la
Serikali alitangazwa anatokea Zanzibar, aligeuzwa na kuonekana kuwa
anatokea Tanzania Bara. Mjumbe mwingine, Zakhia Meghji wa CCM anatokea
Tanzania Bara lakini tumeelezwa kuwa anatokea Zanzibar,” alisema.
Katika hatua nyingine, wakati Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa akidai kuwapo kwa mpango wa ununuzi wa
helikopta tatu za Serikali kwa malengo ya kuzitumia kuisaidia CCM kwenye
Uchaguzi Mkuu ujao, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue amesema madai
hayo siyo ya kweli.
Jana, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, Dk Slaa alidai kwamba kuna
mpango wa ununuzi wa helikopta tatu za Serikali ambao unapangwa kufanywa
bila kufuata taratibu za ununuzi na kwamba Rais Jakaya Kikwete akienda
ziarani China ataiona mojawapo.
Alidai kwamba helikopta hizo zitakazonunuliwa kwa
mkopo kutoka Serikali ya Ujerumani, zitanunuliwa Ufaransa lakini wakala
anayetumika kuzinunua anatuhumiwa nchini kwa ufisadi, alisema wakati
ukifika atataja jina la wakala huyo.
Mbali na helikopta hizo, Dk Slaa pia alidai kuwapo
kwa mpango wa kununua mitambo maalumu ya kunasia sauti za viongozi wa
Chadema.
Hata hivyo, Balozi Sefue katika maelezo yake
alisema: “Ni kweli kwamba Rais atakwenda China kwa mwaliko wa Rais wa
nchi hiyo, lakini haendi kuangalia chopa”.
Katibu Mkuu Kiongozi aliweka wazi kuwa yapo mawazo
ya kununua helikopta hizo kwa ajili ya matumizi ya jeshi lakini uamuzi
bado haujafanyika.
“Hata kama uamuzi utafanyika kwamba zinunuliwe kwa
ajili ya kuliwezesha jeshi letu (nasisitiza, bado uamuzi haujafanyika
sasa) haiwezekani kusafirisha helikopta kwenda China kwa sababu ziara ya
Rais haihusiani kabisa na suala hilo,” alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema kauli
ya Dk Slaa ni uzushi na uongo na kwamba ajifunze kusema kweli... “Ni
kiongozi na tunamheshimu kwa hiyo lazima ajifunze kusema kweli. Haiingii
akilini kusema kwamba helikopta inaweza kusafiri kilometa zote hizo
kwenda kumfuata Rais China eti akaione, kwani Rais ni injinia au ni
nani?
Halafu technically (kiufundi) ni jambo lisilowezekana”. Umbali kutoka Paris Ufaransa hadi Beijing, China ni kilometa 8,022.
Uchaguzi Mkuu
Akigusia ununuzi wa mitambo ya usalama
itakayotumiwa na Jeshi la Polisi, huku akionyesha nyaraka ya serikali
yenye maelezo ya ununuzi huo iliyoandikwa na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (jina limehifadhiwa) alisema:
“Rais ameomba kwenda Beijing kwa ajili ya kuona
mitambo ya kiusalama ya polisi. Cha kushtusha zaidi katika nyaraka hii
inaeleza mitambo hiyo lazima iwe imefika haraka iwezekanavyo kabla ya
Uchaguzi Mkuu kwa sababu tunaogopa kuna vurugu zitatokea. Hayo yamesemwa
kwenye maandishi wa Serikali,” alisema.
Alisema aliyeandikiwa nyaraka hiyo ni Waziri wa
Mambo ya Nje na kufafanua kuwa nyaraka hiyo iliandikwa Oktoba7, 2014 na
mawasiliano kati ofisa huyo na Waziri yalifanyika saa 11 jioni.
Katika mkutano wake Dk Slaa pia alisema: “Rais
anaambiwa kwamba ndege ya Jeshi anayotaka kununua ipo kwenye mji
mwingine, mji huo haupo katika eneo la ziara yake, lakini wanawaambia
wahusika kule China, ndege irushwe na iletwe mpaka Rais atakapokuwa ili
aione mwenyewe. Hivi Rais ni ofisa mnunuzi au!” alihoji.
Akizungumzia hilo safari hiyo, Msemaji wa Wizara
ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally alisema: “Hatuna taarifa kama Rais
anakwenda Beijing.”
Kuhusu madai ya Rais kukagua vifaa vya kiusalama
vya polisi na helikopta zinazodaiwa kuwa zitanunuliwa Mkumbwa alisema:
“Hayo ni madai ya kufikirika kwa kuwa Rais siyo ofisa ununuzi.” Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment