Friday, January 03, 2014

WARIOBA: SERIKALI TATU SI MZIGO

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, ametetea muundo wa serikali tatu kuwa hauna gharama, tofauti na inavyotafsiriwa na wengi. Mbali na kutetea gharama za uendeshaji wa serikali tatu, Jaji Warioba pia amewashukia wanaodhani mapendekezo ya muundo wa serikali tatu ni yake binafsi, kutokana na msimamo wa siku nyingi wa kiongozi huyo.
 
 Akizungumza na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Jaji Warioba alisema muundo wa serikali tatu umepunguza gharama za uendeshaji. Kwa mujibu wa Jaji Warioba, chini ya muundo huo hata Bunge linatarajiwa kuwa na wabunge 75 tu, hatua ambayo itapunguza gharama. Mwenyekiti huyo alisema kuwa gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano zitakuwa katika Wizara ya Ulinzi na Usalama pamoja na Mambo ya Nje huku katika maeneo yaliyobaki gharama zake zitakuwa zimepungua zaidi. 
“Hivi kwa nini hili la muundo wa muungano tunajadili gharama wakati kila mwaka tunapoongeza mikoa, wilaya, tarafa, majimbo na vijiji gharama zinaongezeka wala hakuna anayezungumzia wala kuhoji? Hivyo hivyo kwa kuwa na serikali tatu, hakuna gharama, tena kimsingi tumepunguza gharama za migogoro ya mara kwa mara ya kushughulikia kero za Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Mwenyekiti huyo wa tume ambaye alitumia muda mwingi kufafanua mambo mbalimbali, alisema suala la mgawanyo wa mikoa ikiwemo wanaopendekeza Jijila Mbeya ligawanywe pamoja na Songea, kuna gharama kubwa za uendeshaji. 

“Hivi mnajua namna gani viongozi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Tanzania Bara wamekutana kujadili matatizo ya Muungano? Gharamawanazotumia mnazifahamu?” alihoji. Alisema kuwa hata kuwepo kwa serikali mbili bado hakutapunguza gharama, hivyo ni muhimu kukubaliana na mawazo ya wananchi juu ya muundo wa serikali tatu ambazo zimepunguza gharama. 
Mwenyekiti huyo alisema Serikali ya Muungano itakuwa na chanzo chake cha mapato ambayo hayatokani na kodi. Alisema kuwa gharama itakayoendesha Serikali ya Muungano ni ile inayohusu mambo ya utawala ambayo ni ndogo.
Akizungumzia baadhi ya makada na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaomlaani kwa kuingiza hoja ya muundo wa muungano kwenye rasimu, Warioba alisema rasimu hiyo si yake bali ni maoni ya Watanzania.
Alisema wananchi wameona sababu za kuwepo serikali tatu na tume imechambua na kuona kuwa kuna hoja za msingi za kuwapo muundo wa serikali tatu. “Wanaotafsiri rasimu hii ni lazima waelewe kuwa wanatafsiri maoni ya wananchi, si ya Warioba, hatutaki sisi kuhusishwa na vyama maana tumefanya kazi kama walivyosema Watanzania ambao wanataka serikali tatu,” alisema.
 Alisema kuwa anashangazwa na maoni yanayotolewa na baadhi ya wachache kuwa tume imemgeuka hayati Mwalimu Julius Nyerere. “Sijui hawa wanafikiri Mwalimu angekuwa na mawazo mgando wakati wote,” alisema huku akitolea mfano Nyerere alivyokubaliana na ripoti ya Jaji Nyalali ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi huku wengi wakikataa.
Alisema kuwa masuala ya Muungano yameanza kufanyiwa mabadiliko wakati Nyerere akiwa hai, akitolea mfano mwaka 1977 makusanyo ya kodi ya Zanzibar yalivyopendekezwa kubaki huko. 
Warioba alisema kuwa mwaka 1984 ilipitishwa sheriana Zanzibar kuwa kodi yoyote itakayopitishwa na Bunge au sheria yoyote ni lazima ijadiliwe na Baraza la Wawakilishi. Katiba ya Tanganyika Warioba alisema kwa kutumia sheria za Local Government na kupitia Hansard, Katiba ya Tanganyika itaweza kupatikana ndani ya kipindi kifupi kisichozidi
miezi mitatu. 
Alisema hakuna haja ya kutumia fedha nyingi kupata mawazo mapya ya kuanzishwa kwa Katiba hiyo. Mwenyekiti huyo alisema ili kuhakikisha Katiba mpya inatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao ni lazima kuna muundo wa vitu vitakavyobadilika ikiwemo Tume ya Uchaguzi. “Ukishakubali Katiba hii lazima uunde Tume Huru ya Uchaguzi na katika hilo naona hakuna tatizo na nilishasema kutunga Katiba ya Tanganyika si kazi ngumu,” alisema. 
Alisema kuwa ukisoma rasimu ya pili ukurasa wa kwanza hadi wa tano ni maoni yanayotokana na mawazo ya Watanzania, hivyo hakuna jambo ambalo linaweza kubadilika katika maoni ya maadili, malengo, haki za binadamu na mamlaka ya wananchi. Kuwania uongozi Jaji Warioba alisema kutokana na maoni ya wananchi, viongozi waliostaafu hawatakuwa na haki ya kuwania uongozi wowote wa kisiasa hadi ipite miaka mitatu tangu kustaafu kwao. 
Aliwataja wanaoangukia katika sheria hiyo kuwa ni Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Juu, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na wajumbe, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. “Usipofanya hivyo hao hawatakuwa ‘active’ ni lazima wakisha staafu ipite miaka mitatu ndiyo waruhusiwe kuwania nafasi za uongozi,” alisema. Alisema kuwa wananchi wamefikia uamuzi huo baada ya wastaafu walio wengi kukimbilia siasa baada ya kustaafu. 
Mikopo kwa viongozi Alisema kuwa Katiba inazuia matumizi mabaya ya vyeo hivyo kiongozi wa umma hapaswi kutumia madaraka yake na kukopa mikopo katika taasisi za kifedha. “Katiba inazuia matumizi mabaya ya vyeo, katika rasimu tumeweka ile miiko lakini sheria itakuja na kutaja ni viongozi wapi wanahusika katika hilo,” alisema. 
Warioba alisema kuwa wamezuia viongozi kutumia madaraka yao kupata mikopo bali anaweza kukopa kwa utaratibu wa kawaida. Uraia Jaji Warioba alisema kuwa rasimu ya kwanza haikuzungumza juu ya uraia bali kwa sasa imezungumzwa na kuwekwa kwa aina yake. 
Alisema kuwa kwa sasa Mtanzania anaweza kupata uraia wa nchi mbili (kinasaba) bila kupoteza haki zake. “Sawa hawezi kuwania urais lakini kuna haki za msingianazopaswa asipoteze,” alisema. Ukomo wa Tume Alisema kuwa tume itakamilisha kazi yake itakapowasilisha rasimu hiyo katika Bunge la Katibakutokana na muongozo wa sheria unavyoainisha. 
Mwenyekiti huyo alisema kuwa sheria iliweka wazi watu gani wanaostahili kuingia katika Bunge hilo, hivyo tume hiyo itabaki kuwa mshauri. “Sisi kazi yetu itabaki kuwa washauri na si kuwa wabunge, tunafuata kama sheria inavyosema, hivyo wakitaka ushauri tutawapa lakini kazi kubwa tumekamilisha,” alisema.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...