Wednesday, October 16, 2013

RAIS WA ZANZIBAR DKT. SHEIN ASISITIZA AMANI BARAZA LA IDD ZANZIBAR

DSC_0112
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein wapili kushoto akiomba Dua pamoja na viongozi wengine wa Kitaifa katika Swala ya Idi –El-Hjji ilioswaliwa Kitaifa huko katika kitongoji cha Marumbi Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja.kulia kwake ni Kadhi Mkuu wa Zanzibar Khamis Haji Khamis na kushoto yake ni Katibu mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdalla Twalib,Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanizbar Maalim Seif Sharif Hamadi na wamwisho ni Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmod Mussa Wadi. DSC_0230
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohd Shein akitoa hotuba katika baraza la Idi -El-Hajji lililofanyika huko Tunguu Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja DSC_0206
Baadhi ya Viongozi na Wananchi waliohudhuria katika Baraza la Idi-El-Hajji lililofanyika huko Tunguu Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja
PICHA ZOTE NA YUSSUF SIMAI ALI-HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ameendelea kusisitiza hali ya Amani na kukemea Vitendo vinavyofanywa na baadhi ya Watu wachache wenye lengo la kuiharibu sifa ya Zanzibar.
Amesema tangu Karne zilizopita Zanzibar pamekuwa pahala pa Amani na utulivu na hivyo kuitaka jamii kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuwafichua watu ambao wanaoharibu Amani iliyopo.

Rais Shein ameyasema hayo leo katika Hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd lililofanyika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kiujumla hali ya Amani na Utulivu imetanda kote katika Visiwa vya Zanzibar hali inayopelekea Serikali kupanga na kutekeleza mipango yake ya kimaendeleo kwa lengo la kuimarisha uchumi na ustawi wa Wananchi wake.
Hata hivyo amekea tabia inayofanywa na baadhi ya Watu wachache wanaowahujumu na kuwatia hofu Wananchi pamoja na Wageni wanaoitembelea Zanzibar.
Amefahamisha kuwa hakuna Dini inayowaelekeza waumini wake kuwahujumu Wanadamu wengine na kwamba watakaobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amewahahakikishia Wananchi na Wageni kwamba vyombo vya Ulinzi na usalama vinafanya kazi nzuri ya kusimamia ulinzi na Usalama na kuitaka jamii kutoa ushirikiano unaohitajika.
Aidha Dkt. Shein amebainisha kuwa kutokana na kuimarika kwa hali ya usalama na amani Uchumi wa Zanzibar unaendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha kutoka Asilimia 6.7 kwa mwaka 2011 hadi Asilimia 7.0 mwaka 2012.
Ameongeza kuwa hali hiyo inatoa matumaini makubwa hasa ikizingatiwa kuwa ukuaji wa uchumi katika Bara la Afrika ni Asilimia 5.3  ambapo kwa upande wa Ukuaji wa uchumi wa Dunia ni Asilimia 2.9
Kuhusu Zao la Karafuu Dkt. Shein amesema kuwa Shirika la Biashara la Taifa ZSTC linatarajia kununua tani 4,016 kwa mwaka 2013 na kuwaomba Wananchi waendelee kushirikiana na Serikali katika kupambana na watu wanaofanya Magendo ya Karafuu.
Awali Akimkaribisha Rais Shein kutoa Hotuba yake Waziri wa Katiba na Sheria Aboubakar Khamis Bakary alisema Serikali imepanga Sala na Baraza la Idd katika Siku kuu zote za IDD-EL HAJJ zitakuwa zikifanywa kitaifa katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba ambapo kwa mara hii Swala ya Idd ilifanyika kijiji cha Marumbi Mkoa wa Kusini Unguja.
alifahamisha kuwa Serikali imeamua kufanya hivyo ili Wananchi wa Mikoa yote ya Unguja na Pemba wapate fursa ya kuswali pamoja na Viongozi wao Wakuu wa Kiserikali lakini kwa upande wa Swala ya IDD EL-FITRI itaendelea kuswaliwa kitaifa katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Sherehe ya IDD EL HAJJ inakuja kila mwaka kufuatia kumalizika kwa Ibada ya Hijja inayofanyika MAKKA Nchini Saudia kwa Waislamu wenye uwezo wa kufanya Ibada hiyo.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR  16/01/2013

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...