Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa kwa muda baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi
kwenye wodi binafsi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) alikolazwa
jana, Sheikh Ponda alisema kutokana na hali hiyo hakumbuki matukio yaliyofuata
baada ya hapo.
“Sikumbuki hata nilipata huduma ya kwanza hospitali
gani kwa sababu sikuwa katika hali ya kawaida. Mambo mengine yaliyotendeka kabla
ya kujeruhiwa ninayakumbuka vizuri,” alisema Ponda ambaye inasadikiwa kwamba
alipigwa risasi ya begani, Ijumaa iliyopita mjini
Morogoro.
Alisema alihutubia katika Kongamano la Waislamu kwa
muda mfupi akizingatia muda uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano huo na baada ya
hapo alishuka na kupanda kwenye gari binafsi ambalo lilizingirwa na polisi ndipo
akaamua kushuka na kuanza kutembea kabla ya kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh
Ponda
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya kwanza mara baada
ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi?
Jibu: Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea mbele kwa
hiyo haikubaki mwilini wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo maana
kulikuwa na purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya
kwanza?
Jibu: Kwa kweli kwa sasa siwezi kukumbuka nilihudumiwa
wapi kwa sababu mara baada ya kujeruhiwa sikuwa katika hali yangu ya kawaida,
nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa
risasi?
Jibu: Bahati nzuri ni kwamba tukio hili lilitokea
kweupe wapo wengi walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia kuthibitisha na
ushahidi mwingine ni jeraha hili.
Swali: Nini msimamo wako baada ya
tukio?
Jibu: Nitaendelea kuzungumzia haki za Waislamu na
siwezi kurudi nyuma. Pamoja na kwamba wananiona mimi ni mtu mchochezi lakini
wanaeneza chuki dhidi yangu kwa njia wanazojua wao. Nitaendelea, risasi
haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar,
unalizungumzia vipi hilo?
Jibu: Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi dhidi ya
viongozi wa Kundi la Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi tisa sasa, kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina dhamana, sasa nikauliza
kwa hao viongozi, kwa nini hawazingatii sheria? Kesi zina muda mrefu hazitolewi
uamuzi, nikawasisitiza wazingatie misingi ya sheria kwa kuwa hivyo
wanavyowatendea wananchi wajue kwamba hawastahili kupewa tena ridhaa ya kuongoza
nchi, nilifikisha ujumbe wangu.
Swali: Kuna tukio la kumwagiwa tindikali mabinti wawili
wa Uingereza lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa, hili
unalizungumziaje?
Jibu: Sijaona huo ushahidi ambao wanahangaika
kunihusisha na tukio hilo, nahusishwa vipi? Matukio ya kumwagiwa tindikali
yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara huko kabla sijakwenda kuhutubia. Vyombo vya
dola vifanye kazi yake vyema ili kubaini ukweli wa jambo
hili.
Pia Mwananchi ilizungumza na mke wake, Sheikh Ponda,
Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa
mumewe.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la kujeruhiwa kwa
mumeo?
Jibu: Hili ni dhumuni la Serikali, lililenga moja kwa
moja kumdhuru ili kunyamazisha harakati zake za kutetea wanyonge. Ni tukio la
kupangwa, halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia sana hivyo ililenga
kumnyamazisha.
Namshauri Rais (Jakaya Kikwete), kuhakikisha kwamba
haki za wanyonge zinawafikia, asije akafikiri hili lililotokea kwa Sheikh Ponda
ni suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo ili kuweka
mabadiliko.
Alivyowaponyoka polisi
Mtu wa karibu wa Sheikh Ponda alisimulia jinsi
walivyomsafisha kiongozi huyo kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na kukwepa
vizuizi vya polisi ambao walikuwa wakiendelea kumsaka.
“Msafara ulikuwa na magari mawili. Moja lilitumika kwa
uangalizi, lingine lilimbeba Sheikh Ponda. Tulipofika Chalinze tulikuta kizuizi
tukakikwepa kwa kupitia Msata kisha Bagamoyo hadi Dar es Salaam na kumfikisha
Muhimbili,” alisema.
Waigomea polisi
Msemaji wa familia ya Sheikh huyo, Isihaka Rashid
alisema hawaitambui tume iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo
linalotuhumiwa.
“Tunachofanya hivi sasa ni kukusanya ushahidi wetu, kwa
bahati nzuri tayari tumepata mkanda wa tukio lenyewe ambao utatuwezesha kumbaini
aliyemshambulia Sheikh Ponda.
“Hatuwezi kuhitaji majibu ya hiyo tume yao na hata leo
kuna maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu na Kituo cha Kati, Dar es Salaam
walifika wakitaka kumhoji eti kuhusu uchochezi lakini alikataa kuzungumza hadi
mwanasheria wake awepo, wakaondoka,” alisema Rashid.
MWANANCHI