Tuesday, August 06, 2013

NI AIBU TANZANIA KUWA KITOVU CHA DAWA ZA KULEVYA....!!!

Dk. Harrison Mwakyembe.

KWANZA kama ilivyo ada tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuiona siku ya leo, hakika anatupenda sote na hana ubaguzi.
Baada ya kusema hayo tugeukie mada ya leo. Nchi hii miaka nenda rudi tumekuwa na sifa moja kubwa kuwa taifa lenye amani na utulivu miongoni mwa mataifa katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.
Sifa hiyo sasa imegeuka na kuonekana sisi ni mabingwa wa kusafirisha dawa za kulevya. Hakika hili la kubobea katika biashara ya dawa za kulevya siyo sifa ya kujivunia hata kidogo mbele ya mataifa.

Hakuna siri wala kificho kwamba Tanzania sasa imejizolea medani za aibu kimataifa kwani katika miaka ya hivi karibuni, imekuwa na  sifa ya kuwa moja ya vinara wa biashara ya dawa za kulevya duniani.


 Ni aibu na ni sifa inayochafua taswira ya nchi yetu, kwani hivi sasa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi wanaficha nyuso zao kwa aibu kutokana na upekuzi wa aina yake wanaofanyiwa na mamlaka za forodha na uhamiaji katika nchi wanazopitia.


 Msafiri mwenye pasi ya kusafiria iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila anapoingia katika nchi ya kigeni anapata msukosuko mkubwa wakati wa ukaguzi.
Hali hiyo imetokana na matukio ya Watanzania wengi kukamatwa ughaibuni wakiwa na dawa hizo, kusema kweli haya ni matukio yanayotoa taswira ya taifa linaloanza kupotea njia.
 Kila Mtanzania atafakari, katika kipindi cha wiki mbili tu, Watanzania wanne wamekamatwa katika nchi mbalimbali wakiwa na dawa hizo na wakiwa wametokea Tanzania! Yaani wanapitisha dawa hizo kama vile wamechukua sukari na vyombo vya kudhibiti vipo.

Tukumbuke kuwa mwezi uliopita, wasichana wawili Watanzania walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Shilingi bilioni 6.8 wakitokea Dar es Salaam.
Mpaka leo hakuna anayejua jinsi shehena hiyo kubwa ilivyoweza kupita Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini  Dar es Salaam bila kugunduliwa na mamlaka husika ambazo zimepatwa na kigugumizi kuhusu tukio hilo baya. Hivi sasa wasichana hao wamefunguliwa mashtaka nchini humo.
Kama vile hiyo haitoshi, Watanzania wengine wawili wiki iliyopita walikamatwa Hong Kong, China wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Shilingi bilioni 7.6 nao wakitokea Dar es Salaam kupitia Dubai. Maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA) wamesema kwamba katika wiki hiyo, walimkamata kijana mwenye miaka 26 akitokea Tanzania akiwa na dawa za kulevya kilo 1.6 aina ya heroin zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5.
Cha kushangaza ni kwamba siku hiyohiyo jioni, wakamkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 akiwa amemeza gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Tatizo la biashara ya dawa za kulevya hapa nchini limekuwa kubwa, kwani takwimu zinaonyesha kuwa, kuna orodha kubwa ya Watanzania waliokamatwa ughaibuni wakiwa na dawa hizo na wengi wao wanasubiri kunyongwa.

 Jambo la kusikitisha ni kuwa tumekuwa tukiambiwa kwamba kwa muda mrefu serikali imekuwa na orodha ya magwiji wa biashara ya dawa hizo lakini imekuwa ikishikwa na kigugumizi cha kuwachunguza kisha kuwataja au kuwafungulia mashtaka.
Mbaya zaidi ni kwamba hata pale baadhi yao walipofunguliwa mashtaka, kesi zao zimekuwa zikipotea hivihivi tu pasipo maelezo. Hakika ipo haja ya kuanzisha mahakama kwa ajili ya janga hili na wateuliwe mahakimu na majaji maalum.

Mimi na Watanzania wenzangu wanaoitakia mema nchi hii, naamini katika hili serikali inastahili kubeba lawama kwa kutowashughulikia magwiji wa biashara hiyo ambao naamini wanaokamatwa watakuwa wanawataja.

 Lazima tutambue kwamba Watanzania wanaokamatwa na dawa hizo hapa nchini na huko ughaibuni ni dagaa tu, kwani mapapa wenye biashara hiyo wamekaa kando na wanapokamatwa hao wasafirishaji, huandaa wengine wapya, sasa tunajiuliza kwa nini serikali inakaa kimya?

Wengi tulishituka tuliposikia mwishoni mwa wiki, katika mhadhara wa kongamano la kidini lililofanyika jijini Mbeya, vijana wawili waliokuwa wakitumiwa kusafirisha dawa hizo, walisalimisha kilo tano za dawa aina ya heroin baada ya kuguswa na mahubiri ya mhubiri katika kongamano hilo.

Uzuri ni kwamba vijana hao waliyataja majina ya wamiliki wa dawa hizo, wakiwamo baadhi ya mawaziri na wabunge.
Naamini hao ni baadhi ya mapapa wa dawa za kulevya hapa nchini na ndiyo wanaotufanya tuwe taifa la wauza unga. Muda umefika sasa washughulikiwe, Wizara ya Mambo ya Ndani chini ya Dk. Emmanuel Nchini wahimizeni polisi na uhamiaji, wizara ya usafirishaji chini ya Dk. Harrison Mwakyembe wakodoleeni macho Mamlaka ya Uwanja wa Ndege (TAA),  ni wakati wenu kuhakikisha nchi haichafuki kwa dawa za kulevya.
CHANZO GPL

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...