Wednesday, July 17, 2013

HIKI NDICHO KILICHOIMALIZA TAIFA STARS DHIDI YA UGANDA...!!!

 

Mshambuliaji wa timu ya Taifa Stars, Mrisho Ngassa (katikati) akijaribu kuwatoka mabeki wa Uganda, katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za CHAN 2014. Uganda ilishinda 1-0. Picha na Michael Matemanga.

KIWANGO cha chini kilichoonyeshwa na wachezaji wa Taifa Stars juzi dhidi ya timu ya taifa ya Uganda, kimewavunja moyo baadhi ya wapenzi wa soka hapa nchini na kujikuta wakipoteza matumaini ya kuiona timu hiyo ikifuzu kushiriki katika fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
 

Hata hivyo kocha mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amewataka kuwa wavumilivu kwani lolote linaweza kutokea katika mechi ya marudiano itakayofanyika nchini Uganda wiki mbili zijazo.

“Suala ni kwamba tulitengeneza nafasi tukashindwa kuzitumia, katika mechi ya marudiano tunatakiwa kutengeneza nafasi na kuzitumia kwani mpira ni magoli,” alisema kocha Poulsen.


Katika mechi hiyo ya marudiano, Taifa Stars ambayo juzi ililala kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, inatakiwa kushinda zaidi ya mabao 2-0 ili iweze kujihakikishia mazingira mazuri ya kufuzu kushiriki fainali hizo za CHAN zitakazofanyika Afrika Kusini ambazo zitakuwa za tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwake.


Katika mechi ya juzi dhidi ya Uganda, wachezaji wa Stars walicheza chini ya kiwango tofauti na walivyocheza dhidi ya Morocco na Ivory Coast wiki chache zilizopita wakati wakitafuta tiketi ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014.


Nguvu na kuchoka

Wachezaji wengi wa Taifa Stars katika mechi hiyo walionekana kutokuwa na nguvu kabisa, pia walichoka mapema ukilinganisha na wapinzani wao.

Mara nyingi kila walipokuwa wakishindana kuwania mpira wachezaji wa Uganda walikuwa wakiibuka na ushindi ingawa walikuwa hawatofautiani sana kwa maumbo.


Hata hivyo kocha mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen alipoulizwa juu ya hali hiyo alisema kuwa pengine imechangiwa na wachezaji wengi wa kikosi hicho kuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 
Kusoma mchezo

Hilo pia lilikuwa ni tatizo kwa wachezaji wa Stars kwani hakukuwa na uwezo wa kuusoma mchezo na kutafuta mbinu mbadala za kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo tofauti na ilivyo kuwa kwa wenzao wa Uganda ambao kipindi cha pili walibadili mfumo na kupata bao la mapema.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...