Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage.
Na Saleh Ally
UONGOZI wa kampuni ya Bakhresa inayomiliki klabu ya Azam umemwaga dola
milioni moja (zaidi ya Sh bilioni 1.6) ili kupata haki ya udhamini wa Ligi Kuu
Bara kama warushaji wa matangazo ya televisheni.
Kutokana na kumwaga fedha hizo, kampuni hiyo
kupitia kituo chake kipya cha televisheni yake ya Azam TV, kitakachoanza kurusha
matangazo hivi karibuni, kitapewa haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu
Bara.
Kampuni hiyo iliyokuwa inapambana na Supersport
ya Afrika Kusini iliyokuwa tayari kutoa dola 500,000 imeihakikishia bodi ya ligi
hiyo kuwa iko tayari kutoa fedha hizo na kila klabu zikiwemo Yanga na Simba
zitapata Sh milioni 140 kila moja kwa msimu.
Pamoja na fedha hizo kutoka kwa wamiliki hao wa
Azam FC ambayo ndiyo wapinzani wakubwa wa Simba na Yanga, klabu hizo kongwe
zimesema zinataka kulipwa zaidi kwa kuwa ndiyo zenye mashabiki wengi.
Katika kikao kilichofanyika juzi, kumezuka
mjadala mkubwa huku Simba na Yanga zikisisitiza kwamba haitakuwa haki zenyewe
kupewa Sh milioni 140 sawa na klabu nyingine ambazo zina mtaji mdogo wa
mashabiki.
“Lakini watu wa bodi ya ligi wameonyesha
kutokuwa waungwana maana wameendelea kulazimisha Simba na Yanga zilipwe sawa na
klabu hizo ndogo. Sisi tunaona hii si sahihi,” kilieleza chanzo cha
uhakika.
Chanzo kingine kimeeleza, uamuzi huo wa kampuni ya
Bakhresa kupewa nafasi kulikuwa kunapingwa ‘kiana’ na watu wa klabu hizo kubwa
bila ya kujali inatoa fedha nyingi mara mbili ya SuperSport kwa madai eti ni
kubwa na wataonekana nchi nyingi.
Lakini wajumbe wengine walisisitiza suala la
fedha lipewe kipaumbele na fedha nyingi ndiyo zichukuliwe, hapo ndipo kukaibuka
suala la mvutano wa Yanga na Simba kutaka kupewa zaidi.
Taarifa zinaeleza tayari ufungaji wa mitambo ya
Azam TV inaendelea kwa kasi ya ‘kimondo’ na baada ya siku kadhaa itaanza kazi
huku ikitumia mitambo ya kisasa zaidi nchini. Kwa hisani ya GPS
No comments:
Post a Comment