RAIS
Jakaya Kiwete akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa
serikali na dini wakati alipohudhuria sherehe za miaka 25 ya Askofu wa
jimbo kuu la Morogoro Telesphol Mkude wa pili kulia kwa rais katika
viwanja vya shule ya ST Peter mkoani Morogoro jana.
SIKU
chache baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutaka Serikali iachwe ifanye
kazi yake katika kudhibiti vurugu zinazoibuka kila kukicha, Askofu wa
Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Telesphor Mkude naye
ameitaka Serikali kuwadhibiti wote wasiotaka nchi itawalike.Askofu huyo amesema kuonya pekee hakusaidii, bali inawajibu wa kuwachukulia hatua kali ili kukomesha vitendo vinavyotishia amani nchini.Askofu
Mkude aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25
ya uaskofu wake kwenye viwanja vya Seminari ya Mtakatifu Petro mjini
hapa ambapo Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri
waliohudhuria.
Katika maadhimisho hayo, maaskofu zaidi ya 35 wakiwemo wa Majimbo Makuu wa ndani na nje ya nchi walihudhuria.
Aidha
walikuwapo mapadri, watawa, waamini na mamia ya wananchi wa mikoa ya
jirani, sambamba na viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wakiwemo wa
chama tawala, CCM.
Pamoja
na ushauri wake, Askofu Mkude pia alimshukuru Rais kuweza kushiriki
katika maadhimisho hayo, huku alirudia kumwomba yeye pamoja na Serikali
yake kusimamia suala zima la amani ya Tanzania.
Askofu
Mkude alisema Serikali inao wajibu kuhakikisha amani inaendelea
kudumishwa wakati wote na kuchukua hatua za haraka za kukutana na
viongozi wa dini pale panapotokea kutoelewana katika imani zao ili
kufikia mwafaka utakaodumisha amani ya Tanzania.
“Suala
hili la kuchinja ...linaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa viongozi
wa dini na Serikali kukutana na kuliweka sawa...mbona hatugombani kwenye
kuzika, makaburi ...hili la kuchinja kwanini linakuzwa zaidi wakati huu
, ambako huku nyuma halikuweza kuwepo ...” alihoji Askofu Mkude mbele
ya Rais.
Naye
Rais Kikwete, akizungumza, aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini
nchini kuendelea kuhubiri amani, upendo, utulivu na mshikamano ili
kujenga misingi imara ya maelewano yaliyodumu kwa miaka mingi miongoni
mwa Watanzania.
Pamoja
na kuomba viongozi wa dini kuhubiri amani, Rais Kikwete alisema
Serikali itaendelea kushirikiana na Madhehebu ya dini katika kuleta
maendeleo ya wananchi ili kuinua hali zao za kimaisha.
Mbali
na hayo Rais Kikwete pia alisema viongozi wa madhehebu ya dini wanayo
nafasi kubwa na ya kipekee ya kuwafundisha vijana kuwa Wacha-Mungu na
raia wema wa nchi yao.
Katika
hotuba yake pia alimpongeza Askofu Mkude kwa kutimiza miaka 25 ya
uaskofu na kusema yeye pia ni miongoni mwa wakazi wa Parokia ya Lugoba,
Wilaya ya Bagamoyo ambayo ni sehemu ya Jimbo la Kanisa Katoliki la
Morogoro.
Rais
pia alisema Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro limetoa fursa kwa maelfu
ya vijana kupata elimu kwa manufaa yao sambamba na kuanzisha vituo vya
afya ikiwa ni juhudi za kuunga mkono mpango wa Serikali za kupunguza
vifo vya watoto na akinamama wajawazito.
Kwa
upande wake, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliwataka viongozi wa
Kanisa hilo, wanapobanwa na hali ngumu ya kutukanwa na watu wengine,
jukumu lao ni kumkimbilia Yesu Kristo huku wakiendelea kuhubiri upendo
na amani.
“Sisi
Viongozi wa Kanisa letu akiwemo Askofu Mkude tunapokumbana na hali ya
ugumu wa kutukanwa na watu wengine ni vyema kuwa karibu na Yesu ili
tuache mahangaiko na badala yake tuhubiri amani na upendo miongoni mwa
waamini na jamii nzima,“ alisema Mwadhama Kardinali Pengo.
Hata
hivyo alimtaka Askofu Mkude kutumia nafasi ya Jubilei hiyo si tu
kumshukuru Mungu kwa kutekeleza mema pia kumwomba radhi Mungu kwa yale
ambayo hakuweza kuyatekeleza na kuwataka waamini wa Jimbo hilo kuendelea
kumpatia ushirikiano katika majukumu yake.
Naye
Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu,
Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye ni Askofu wa Jimbo la Iringa na Msimamizi
wa Kitume wa Jimbo la Songea, alisema upendo ndiyo jambo kuu katika
kusukuma gurudumu la kuwatumikia wananchi na waumini wa Kanisa hilo.
Hivyo
aliwataka Maaskofu na waamini wengine pamoja na wananchi kuendelea
kumwombea Askofu Mkude aweze kutimiza majukumu yale pamoja na Taifa kwa
ujumla.
Wakati
huo huo Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, limetoa zawadi ya fedha Sh
milioni 25 pamoja na kununua matairi matano na kumkabidhi Askofu Mkude
kwa kutimiza miaka 25 ya uaskofu.
Makamu
wa Askofu wa Jimbo hilo, Padre Patrick Kung’alo, alibainisha hayo
wakati akisoma risala ya Jimbo hilo mbele ya wageni waalikwa akiwemo
Rais Jakaya Kikwete.
Kwa
mujibu wa Makamu huyo wa Askofu pia Umoja wa Mapadri wakati wa
maadhimisho hayo ya Jubilee umezindua usajili wa Bima ya Afya ambapo
katika hatua ya awali umetoa kiasi cha Sh 7,890,000 kwa ajili ya
kuwalipia mapadre 23 kwa kadi ya kijani.
Akizungumzia
mafanikio mengine ya kimaendeleo chini ya Askofu Mkude ndani ya kipindi
cha miaka 25 kati ya hiyo 20 akitumika Jimbo la Morogoro na mitano
Jimbo la Tanga, alisema amewezesha kujengwa kwa sekondari 11 za Kanisa ,
Shule za Msingi 12, shule sita za ufundi pamoja na shule 25 za awali.
Makamu
wa Askofu huyo alitaja mafanikio mengine katika kipindi hicho ni
kusomesha mapadri wapya 54, uanzishwaji wa Kituo cha Redio Ukweli,
mashirika 27 ya kuhudumia watawa wa Kanisa hilo wa Jimbo la Morogoro.
Padri
Kung’alo, alitaja mafanikio mengine ni upandishwaji wa hadhi ya Kituo
cha Afya cha Mikumi cha Kanisa hilo kuwa Hospitali kamili, ujenzi wa
vituo vitano vya afya, zahanati 10 na kuwezesha kupandishwa hadhi
Hospitali ya Bwagala kuwa Hospitali Teule ya Rufaa.
Hata
hivyo alisema, Askofu Mkude aliwezesha kuanzishwa kwa kituo cha
kuwatunza watoto wenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo ili
kuwezesha kundi hilo kupata huduma muhimu za kijamii ambazo wanakuwa
hawazipati kama elimu na afya.
CHANZO HABARILEO.
No comments:
Post a Comment