*Yajigamba kufanya mashambulio muda wowote
*Watanzania wapewa mafunzo ya ugaidi nje ya nchi
*Polisi nchini wasema vyombo vya ulinzi viko macho
*Mtanzania akamatwa Kenya akihofiwa gaidi
WAKATI wananchi wa Afrika Mashariki wakijawa na hofu ya mashambulio yanayopangwa kufanywa na vikundi vya ugaidi vya Al Qaeda na Al Shabab, imebainika kuna Watanzania waliopewa mafunzo ya ugaidi wanaojiandaa kufanya maovu.
Hayo yamebainika siku chache baada ya wanamgambo wa kundi la Al Shabab kufanya mashambulio katika Jengo la Biashara la Westgate mjini Nairobi na kuua watu zaidi ya 70 na kuacha mamia wengine wakiwa wamejeruhiwa.
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile aliyasema hayo jana katika mahojiano maalumu na MTANZANIA.