Wanachama kadhaa kati ya sitini
wa chama cha upinzani nchini Burundi MSD waliofikishwa mahakamani leo ,
wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hii ni baada ya serikali kuwatuhumu kwa kosa la kusababisha vurugu na kupanga njama ya mapinduzi dhidi yake.Wengine bado wanasubiri hukumu huku kesi zao zikiendelea.
Walikamatwa baada ya kuhusishwa na purukushani iliyotokea tarehe nane mwezi Machi baina ya wafuasi wa chama hicho na polisi.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa leo katika mahakama ya jiji la Bujumbura.
Mawakili wao wamekosoa uamuzi huo wakisema kuwa umekiuka sheria kwa kile wamesema kwamba kuna maombi mengi waliomba kabla ya kesi hii kusikilizwa ingawa hayakuzingatiwa na mahakama.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alilaani hali ya kisiasa nchini humo,akisema kuwa serikali inakandamiza uhuru wa kisiasa, uhuru wa kuongea na watu kukutana.
Bwana Ban alisema kuwa sio jambo zuri kwa polisi kuingilia maandamano ya upinzani.
Agizo hili lilitokana na ghasia za kisiasa kati ya wanaharakati wa upinzani na polisi mapema mwezi huu.
Wiki jana mahakama nchini humo ilimchukulia hatua kiongozi wa chama cha upinzani (Movement for Solidarity and Development party) ambaye pia ni mwandishi habari wa zamani, Alexis Sinduhije na wanaharakati wengine 71 kwa madai ya njama ya mapinduzi.
Serikali pia ilisitisha shughuli zote za chama cha upinzani cha MSD kwa kipindi cha miezi minne baada ya kukishutumu kwa kuzua vurugu.
Chama hicho kimekanusha kusababisha vurugu zozote.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz