Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebatilisha uamuzi wake wa
kubadili mfumo wa upangaji wa madaraja ya ufaulu kwa mitihani ya kidato
cha nne kama ilivyotolewa awali kwa kurudisha daraja sifuri.
Kutokana na uamuzi huo, sasa daraja la tano lililotangazwa wiki iliyopita kuchukua nafasi ya daraja sifuri sasa limefutwa.
Uamuzi huo umetolewa siku nne baada ya wizara hiyo kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kutangaza kuwa serikali imeamua kubadilisha mfumo wa kupanga alama na madaraja ya ufaulu.
Uamuzi wa kushusha alama za ufaulu ulipokewa kwa hisia tofauti na wadau wa elimu nchini ambao walikosoa mfumo huo kwa kueleza kuwa unaipeleka kaburini sekta ya elimu ya Tanzania.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kutoka Dodoma, alisema baada ya kutafakari serikali imeamua kuondoa daraja la tano kama ilivyokuwa imetangaza awali na kurejesha daraja sifuri.
“Kwanza niwaombe radhi Watanzania kwa mkanganyiko huo uliojitokeza ambao ni jambo moja tu limewachanganya, lakini walio wengi wanapongeza mfumo huu wa madaraja, tulichokuja kuharibu ni ‘statement’ ya neno division five,” alisema.