Sunday, November 03, 2013

HOJA YA KUMNG"OA MAKINDA YAPIGWA KOMBORA

makinda_1af6c.jpg
Mchakato wa kumng'oa madarakani Spika wa Bunge, Anne Makinda(pichani) ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla (CCM), huenda usifanikiwe kutokana na vikwazo kadhaa vikiwamo kupingwa na baadhi ya wabunge wenye ushawishi mkubwa katika Bunge.  

Wabunge wameanza kumpinga hadharani kuhusu suala hilo ambalo jana mjadala wake uliyateka makundi ya wabunge waliokuwa wakihudhuria vikao vya kamati mbalimbali wakati wakiwa kwenye mapumziko. Katika viwanja vya Bunge jana, gazeti hili liliwashuhudia Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) na swahiba wake kisiasa, Kangi Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara (CCM) wakikataa kusaini karatasi waliyopelekewa kuunga mkono kung'olewa kwa Spika.

 Baadaye kwa nyakati tofauti walisema "hoja hiyo haina mashiko" na kwamba hawakutumwa na wapigakura wao kuwania posho bungeni.
Wabunge hao walikuwa wakirejea moja ya hoja za Dk Kigwangalla kwamba Makinda amekiuka kanuni kwa kuidhinisha malipo ya Sh430,000 kama posho kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na wajumbe wa kamati nyingine ambao malipo yao ni Sh180,000 kwa siku.
Wengine wanaompinga Kigwangalla ni Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) na yule wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR - Mageuzi), ambao pia walisema hawaoni sababu za msingi za kumwondoa Makinda madarakani.  
Rage kwa upande wake alisema haoni sababu za msingi za kutaka kumwondoa madarakani Makinda, wakati Kafulila alisema hilo ni suala la WanaCCM, kwani hata Spika aking'olewa atakayeziba pengo hilo hawezi kutoka upinzani. "Kama akitoka Makinda ataingia mtu wa opposition (upinzani) yeyote basi ningeweza kusaini, lakini ninachojua ni kuwa kama wakifanikiwa kumtoa watakaa kwenye Party Caucus (kikao cha chama) na watateua mwingine kutoka miongoni mwao na mimi simwamini mbunge yeyote wa CCM," alisema Kafulila.
 Filikunjombe na Lugola Kwa upande wake Filikunjombe alisema hoja ya Dk Kigwangalla imejengwa katika msingi hafifu na kwamba "haizingatii masilahi mapana ya nchi, bali masilahi binafsi kwa mtazamo finyu wenye lengo la kujitafutia umaarufu".
 
"Bunge ni taasisi kubwa ambayo haiwezi tu kuingia katika mtego wa kuenguana kwa sababu ya posho. 
Watu wa Ludewa watanishangaa leo hii wakisikia kwamba eti nimesaini kumwondoa Spika madarakani kwa sababu ya posho," alisema Filikunjombe na kuongeza: 
 "Kama hoja ingekuwa ni kumtoa Spika kwa sababu anaipendelea na kuitetea Serikali bungeni kana kwamba yeye ni waziri, basi hoja kama hiyo mimi ningeweza kuiunga mkono, lakini siyo suala la posho".  
 
Kuhusu hoja kwamba Spika Makinda alikiuka kanuni kwa kumteua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti badala ya kuchaguliwa kwa kura, Filikunjombe alisema wanaopaswa kulalamika kwanza ni wajumbe wa kamati hiyo na siyo mtu mwingine yeyote.
 
  Kwa upande wake Lugola alisema msingi wa hoja ya Dk Kigwangalla ni masilahi binafsi na kwamba ni mapambano ya kuwania kupata kiwango kikubwa cha posho, suala ambalo kwa sasa siyo ajenda ya kitaifa. 
"Kama kweli mtoa hoja angekuwa ana nia ya dhati na uchungu wa nchi hii, angetuunga mkono katika hoja ya kutaka kumwondoa Waziri Mkuu, lakini hakufanya hivyo sasa iweje leo anataka tumuunge mkono katika masuala ya posho?" alihoji Lugola. Wabunge hao walisema fedha wanazipenda, lakini siyo kipaumbele katika kutekeleza yale waliyotumwa na wanaowawakilisha bungeni. 
 
Hata hivyo Dk Kigwangalla aliwapuuza wabunge hao akisema kuwa anayetaka asaini na asiyetaka asisaini na siyo kumshambulia na kumbeza.  
 
Vikwazo vingine Mchakato wa kutaka kumg'oa Spika pia unaweza hata usifike katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na badala yake kuishia Ofisi ya Katibu wa Bunge ambako bado hoja yake inafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi hiyo.  
 
Hadi jana mchana Dk Kigwangalla alikuwa bado hajapokea majibu kutoka ofisi ya katibu huyo na aliliambia gazeti hili kuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alimwarifu kuwa "wataalamu walikuwa bado wanaifanyia uchambuzi hoja yake hiyo". Dk Kashililah kwa upande wake aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa: "Ni kweli hoja yake (Dk Kigwangalla) tumeipokea na tunaifanyia kazi, tukimaliza tutamwarifu matokeo ya uchambuzi wetu".
 
  Wakati Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akisubiri majibu kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge, alisema tayari alikuwa amekusanya saini za wabunge wapatao 110 ambao wanamuunga mkono katika harakati zake. Miongoni mwa hoja za mbunge huyo ni kwamba Spika amekuwa akivunja masharti ya Kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura kwa kuzuia mijadala hiyo. 
Hata hivyo hatua ya Spika Makinda kuruhusu mijadala kuhusu migogoro baina ya wakulima na wafugaji na ile inayohusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili juzi, inaweza kutumika kama kigezo cha kuiweka kando hoja ya Dk. Kigwangalla. 
 
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema katika mazingira hayo, Ofisi ya Katibu wa Bunge inaweza kutumia sababu hiyo pamoja na nyingine za kiufundi kuiweka kando hoja mbunge huyo, na kuzuia isipelekwe katika kamati husika kama kanuni zinavyoelekeza.
 
  Kikwazo kingine ni ukimya wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambayo hadi sasa imekaa kimya, ikiwa ni dalili ya kuwaacha CCM "waumane" wao kwa wao.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...