• ASEMA IMEPOTEZA MATUMAINI KWA WATANZANIA(na Danson Kaijage, Dodoma Tanzania Daima)
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameonyesha wasiwasi wa chama hicho
kushindwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015 iwapo watendaji wake wataendelea na vitendo vya rushwa.
Alisema kuwa kwa sasa chama hicho
kikongwe kimepoteza matumaini kwa Watanzania kutokana na vitendo ambavyo
siyo vya kiungwana vinavyofanywa na watendaji.
Kwa kusisitiza, Kikwete alisema hata
kama CCM itashinda uchaguzi wa 2015, kama tabia walizonazo watumishi na
viongozi ndani ya chama hazitabadilika, ni wazi kuwa hakitapita kwenye
uchaguzi wa 2020.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo mjini
hapa juzi usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa
makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa wa chama hicho nchini nzima.
"Kama hatutabadilika katika suala la
rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na kama mwaka huo
tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena
madarakani.
"Najua rushwa ipo na mnaendelea
kupokea sh laki mbili za 'airtime' (muda wa mawasiliano), ndugu zangu
hatutafika, ama wengine watavuka na wengine kukwama," alisema.
Alisema tatizo la rushwa kwa viongozi
wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea
imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.