Tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeziandikia kampuni za simu waraka wa kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini (simu card) mara moja kuanzia Julai 30, 2013.
Hatua hiyo inatokana na serikali kushindwa kufuta kodi hiyo ya sh 1,000 iliyopitishwa na Bunge kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete baada ya kukutana na wadau wa sekta ya mawasiliano.
Kwa maana hiyo kila anayemiliki laini moja ya simu atakatwa sh 3,000; anayemiliki laini mbili sh 6,000 na anayemiliki laini tatu sh 12,000, lengo ni kuhakikisha serikali inakusanya sh bilioni 178 zitakazopelekwa kwenye bajeti kuu ya serikali.
Watumiaji wa simu sasa watalazimika kulipia kodi hiyo ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba kwa wakati mmoja.
Bunge kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili kusaidia shughuli za bajeti ya Serikali Kuu.