KUNA jambo moja ambalo mashabiki wa
timu ya soka ya Arsenal wa Bongo wanajivunia kwa sasa. Unajua hao
mashabiki wamefanya nini? Wamegeuza kibwagizo cha wimbo maarufu wa
'Personally' unaotamba kwa sasa wakaupa jina la 'Arsenally'.
Wimbo huo ni wa wakali wa muziki wa
Afrika kwa sasa ambao ni Peter na Paul Okoye wa Nigeria. Kimuziki wakali
hao wanajulikana kwa jina la P-Square.
Kwa sasa wamevunja rekodi ya kuwa
wasanii ambao nyimbo zao hazijawahi kuachwa kupigwa kwenye majumba ya
starehe tangu mwaka 2003 mpaka dakika hii unaposoma ukurasa huu.
Mwaka huo ndipo walipozindua albamu yao ya kwanza 'Last Night' ambayo ilitengenezwa na Timbuk Music Label.
Wasikilizaji wazuri wa muziki,
watakumbuka kwamba tangu kutolewa kwa ngoma yao ya kwanza, kila mwaka
wakali hao wanadondosha nyingine na mpaka sasa hawajawahi kupotea kwenye
ramani.
Unaposoma makala haya, wimbo wao bora wa 'Alingo' unatesa na huku 'Personally' ukiendelea kupasua anga vilevile.