Kumekuwa na mjadala mkali kuhusu iwapo Naibu Spika, Job Ndugai alikiuka Kanuni za Bunge katika kushughulikia vurugu zilizotokea Bungeni Alhamisi iliyopita kwa kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Ndugai ambaye alikuwa kiongozi wa shughuli za
Bunge siku hiyo, aliwaamuru askari kumtoa nje Mbowe baada ya kukaidi
amri yake ya kutaka kuketi chini aliposimama kutaka kupewa nafasi ya
kuzungumza, hali iliyozua tafrani bungeni.
Pamoja na mambo mengine Ndugai amekuwa akituhumiwa
kwamba anaminya uhuru wa wabunge wa upinzani kutokana na mapenzi
aliyonayo kwa chama chake, CCM.
Kwa upande mwingine, kumekuwa na lawama kwamba
Mbowe alikosea kukaidi amri ya Naibu Spika kwa kuwa kanuni zinamtaka
mbunge yeyote (hata akiwa waziri), kuketi pale kiongozi wa Bunge (Spika,
Naibu au Mwenyekiti) anaposimama, hivyo kusababisha mtafaruku.