TAARIFA YA UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA ABSALOM KIBANDA IMEWASILISHWA NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013
UTANGULIZI:
Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi.