Baadhi
ya wabunge na wadau wa elimu wametaka Serikali kutoishia kufuta
matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, bali iwajibishe Baraza la Mtihani
Tanzania (Necta) kwa kufelisha wanafunzi.
Akizungumza kuhusu kauli ya Serikali kufuta matokeo hayo jana, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza alisema taarifa ya tume ingekuwa tofauti na ilivyotolewa ilikuwa isababishe vurugu nchini.
“Kauli
hii ya Serikali ndiyo iliyotegemewa na wadau wa elimu, tume wangefanya
vinginevyo tunge-riot (fanya vurugu), kwa sababu matokeo yaliyotolewa
na Necta siyohalisi. Tume imefanya kazi nzuri na kilio cha wanafunzi kimesikika,” alisema Rweikiza na kuongeza:
“Sasa
na hili nalisema bila kificho, Necta lazima wawajibishwe kwa sababu
wanafunzi wanne wamejiua kwa matokeo hayo yasiyo halali, kule kwangu
(Bukoba Vijijini) wanafunzi wamekata tamaa na wanaolewa. Hiyo yote ni
hasara ambayo haina wa kuilipa.”
Aliongeza
kuwa nchi nyingi duniani ikiwamo Marekani, mtihani wa mwisho
hauchukuliwi kama kigezo kwa sababu inategemea mwanafunzi jinsi
alivyoamka siku ya mtihani na kwamba, wanatumia mitihani iliyopita
kufanya tathmini yao.