Kocha
Mkuu wa Azam, Stewart John Hall (pichani) amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia
mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya
timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa
Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu
hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano
ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea
hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye
Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa
faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi
ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally
Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na
rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya
kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu.
Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa
Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio
ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba
13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro
aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu
yake wacheze rafu.
Naye
Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa
faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi
ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini
mjini Mlandizi.
Pia
Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000
baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya
FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi
wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi
dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile
timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika
uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka
jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia
Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake
kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao
dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga.
Nayo
klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake
kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko
katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu
ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini
ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya
kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa
Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo
Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake
kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro
(MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika
mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi
Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia
uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT
Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia
klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika
uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match
meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba,
Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa,
Moro United.
Mchezaji
Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union
alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya
Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka
uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa
vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati
ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred
Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.