Tuesday, December 05, 2017

MBWA WA POLISI WAMUUMBUA ALIEDANGANYA KUWA KAPOLWA MIL. 20 ZA KAMPUNI

Mfanyakazi  wa kampuni ya saruji ya Simba Cement, Edward Ngassa amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kutengeneza tukio la uongo la kuporwa Sh. milioni 20.4 na majambazi jana.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, mbwa wa polisi mwenye mafunzo ndiye aliyegundua udanganyifu huo wa Ngassa nyumbani kwake.

Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa huyo alitengeneza tukio la uongo kwamba ameporwa fedha na majambazi katika eneo la Uhindini karibu na mgahawa wa Sunja.

Kufuatia ripoti ya tukio hilo, Muroto alisema, timu ya upelelezi ilifanya uchunguzi wa kina na kubaini kwamba hakukuwa na tukio la uporaji katika eneo hilo.

“Katika uchunguzi huo tulienda kumpekua kwa kina mtuhumiwa nyumbani kwake na kufanikiwa kukamata fedha zote alizoiba akiwa ameficha kwenye ndoo ndogo ya plastiki na kuweka udongo kisha kupanda ua juu yake ili zisikamatwe kirahisi,” alisema.

Muroto alibainisha kuwa waliweza kuzifichua fedha hizo kwa kutumia mbwa ambaye alikuwa akinusa kwenye maeneo yote na kuzikuta kwenye ndoo ya ua.

“Huyu mtuhumiwa alimpigia simu mwajiri wake akidai kuwa wakati anaelekea benki kuna pikipiki ya majambazi ilimzuia kwa mbele na kumpora hizo fedha,” alisema Muroto.

Katika hatua nyingine, Kamanda Muroto alisema watu wawili wamekamatwa kwa wizi wa betri tatu za minara ya mawasiliano katika eneo la Chang’ombe na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

“Watuhumiwa Eliezel Muhongole ambaye ni fundi na mfanyakazi wa kampuni ya Halotel na Alfredy Mlugu mkulima na mkazi wa Mpunguzi walikamatwa kwa wizi huu,” alisema Muroto.

Mbali na hilo, Muroto alisema watu watatu wanashikiliwa na polisi mkoani humu kwa kukamatwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 16 na thamani ya Sh. milioni 33.2.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni mkazi wa Dar es salaam Hussein Henry (40), na Mussa Ramadhani (35) na Abdalah Ramadhani (32) wote wakazi wa Kondoa.

“Hawa walikamatwa wakiwa wamepakia meno haya ya tembo kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC516 BDC aina Fekon wakitokea Kondoa wakielekea Dodoma mjini,” alisema

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...