Wakati Serikali
ikihaha kuhakikisha inaandika historia mpya kwa kupitisha Katiba
Inayopendekezwa Aprili 30, mwakani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo – Bisimba amesema siku
hiyo itakuwa mwanzo wa Watanzania kudai Katiba Mpya.
Dk Kijo – Bisimba, mmoja wa wanaharakati maarufu
wa haki za binadamu nchini, amesema katika mazingira ambayo mchakato wa
Katiba una dosari nyingi, ilikuwa ni busara kuusimamisha kwanza ili
kujitathmini kabla ya kuendelea na Kura ya Maoni.
Mhitimu huyo wa shahada ya uzamivu ya sheria
kutoka Chuo Kikuu cha Warwick, Uingereza, alisema hayo katika mahojiano
maalumu na gazeti hili yaliyofanyika wiki iliyopita.
“Katiba hata ikiwa nzuri kiasi gani, kama
haitokani na wananchi, haiwezi kukubalika,” alisema Dk Kijo – Bisimba
akisisitiza hoja yake. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshatangaza kuwa Kura
ya Maoni itafanyika Aprili 30 mwakani baada ya Bunge la Katiba
kukamilisha kazi ya kuiandika Oktoba 4, mwaka huu.
Hata hivyo, mchakato huo uliingia dosari baada ya
kundi la wajumbe kutoka vyama vya upinzani na baadhi ya wateule, kususia
vikao vya Bunge la Katiba kwa madai kuwa chombo hicho cha kihistoria
kilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba iliyowasilisha
na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingiza mambo ya CCM.
Mchakato huo uliingia matatani zaidi katika
kutafuta theluthi mbili ili kupitishwa baada ya kuibuka utata wa kura za
wajumbe wa Zanzibar.
Ingawa ilipita, kumekuwa na maswali mengi kuhusu
uhalali wa baadhi ya kura za baadhi ya wajumbe kutoka visiwani, huku
utata mkubwa ukiwa kwenye kura ya Zakhia Meghji ambaye kwenye Kamati za
Bunge la Katiba alishiriki kama mjumbe wa Bara lakini kwenye kura za
kupitisha Katiba alishiriki kama mjumbe wa Zanzibar.
Alipotakiwa aeleze kama anaona kuna matumaini ya
kupata Katika Mpya katika mazingira ambayo Taifa limegawanyika kimtazamo
kuhusu mchakato wenyewe, Dk Kijo – Bisimba alisema mchakato huo una
dosari nyingi, ikiwamo baadhi ya vifungu kuwekwa kama kiini macho ili
kuwadanganya Watanzania.
“Sisi tangu mwanzo tulikuwa na mambo matatu ambayo
tuliyafuatilia kwa karibu kwenye mchakato huo; haki za binadamu,
utawala bora na maadili.
“Hatukuridhika na mchakato wenyewe pamoja na
maudhui yake. Kwenye mchakato tulipinga suala la kuwashirikisha
wanasiasa, tulitaka wanasiasa wawe ni moja ya tatu tu (ya Bunge lote) na
wengine wawe theluthi mbili. Lakini tukapingwa. Hilo la kuwaongeza
wanasiasa ndilo limechangia Bunge kukosa uhalali.”
Dk Kijo – Bisimba alibainisha kuwa idadi kubwa ya
wanasiasa kwenye Bunge la Katiba ndiyo iliyoleta matatizo mengi katika
mchakato wa mabadiliko ya Katiba, likiwamo tatizo la kura kupitisha
Katiba Inayopendekezwa.
“Ili kuunusuru mchakato wa Katiba, tunapaswa kujitathmini,
kinyume chake kutangazwa kupatikana kwa Katiba Mpya kunaweza kuwa mwanzo
wa Watanzania kudai Katiba Mpya.”
Kuhusu makosa yaliyofanywa na Bunge la Katiba
alisema, lilipaswa kutumia Rasimu ya Katika iliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, lakini kinyume
chake likabadilisha maeneo mengi na kuweka kwenye Katiba
Inayopendekezwa ambayo hayakutokana na maoni ya wananchi.
“Kuondoka kwa Ukawa bungeni kusingeleta shida
kwenye mchakato wa Katiba kama waliobaki wangetenda haki. Lakini hawa
sasa wakatumia fursa hiyo kubadilisha kanuni ili watengeneze Katiba
wanayoona inafaa. Kuboresha siyo kuweka viraka. Kama ilivyo kwamba
nikitaka kuboresha gauni langu ninapaswa kulishona na siyo kuweka
vipande vya nguo nyingine,” alisema.
Alisema Katiba Inayopendekezwa pia ina kasoro ya
kutambua haki za binadamu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba... “Haki za binadamu zimeandikwa kwa kalamu ya risasi kwenye
Katiba hii. Sisi hatukuridhika na haki ya kuishi, haki ya afya na
matumizi ya rasilimali. Lakini Bunge halikujali kwa sababu kwenye haki
hizi hakukuwa na vipengele vya namna ya kuzitekeleza. Kwa mfano, kwenye
haki ya kumiliki ardhi, Bunge liliongeza haki za wavuvi na wachimba
madini. Sasa mvuvi na ardhi wapi na wapi? Hapa wanatudanganya na hiki ni
kiini macho.” Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Dk Kijo – Bisimba alieleza kuwa suala jingine
ambalo taasisi hiyo imeona ni kasoro kwenye Katiba hiyo ni kuondoa
kipengele cha mikataba kuridhiwa na Bunge na rais kupunguziwa madaraka
ya uteuzi.
Alisema utaratibu uliowekwa na Tume ya Jaji
Warioba kwamba kuundwe vyombo vya uteuzi, ulikuwa mzuri na ungesaidia
kupunguza uwezekano wa mkuu huyo wa nchi, kuchagua watu kulingana na
masilahi yake.
“Kama kutakuwa na chombo cha uteuzi, halafu majina
yakaenda kwa rais na baadaye bungeni, utaona kwamba walau kuna
udhibiti, lakini ilivyo kwamba rais ateue watu moja kwa moja ni tatizo,”
alisema.
Kuhusu utawala, alisema Bunge limekosea kuondoa
kipengele hicho kwenye Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba
kinachotaka mawaziri wasiwe wabunge, kwani hatua hiyo inawafanya
washindwe kuwajibika serikalini. Pia Bunge limekosea kuendelea kumweka
rais sehemu ya Bunge.
“Rasimu ya Warioba ilitaka Bunge liisimamie
Serikali, lipitie mikataba na mamlaka ya Rais ya uteuzi yapungue. Lakini
wakaondoa hayo yote kwa masilahi yao,” alisema.
Uzalendo
Dk Kijo – Bisimba aliitaja kasoro nyingine kwenye
Katiba Inayopendezwa kuwa ni kuondolewa kwa tunu za Taifa kutoka kwa
wananchi wa kawaida na kuzipeleka kwa viongozi.
“Tunu kama uzalendo, uwajibikaji na nyingine
zimeondolewa na Bunge na kuzipeleka kuwa tunu za viongozi. Sasa utampata
kiongozi mwenye tunu hizo kama hatokani na jamii inayozienzi?” alihoji.
Alisema Taifa lilipofikia, linahitaji kuwa na tunu ambazo
zitakuwa msingi wa maadili, vinginevyo tatizo la mmomonyoko wa maadili
litaendelea na kutishia mustakabali wa Taifa.
50 kwa 50
Akizungumzia uwiano wa jinsia wa 50 kwa 50, Dk Kijo – Bisimba alisema Katiba Inayopendekezwa imeondoa dhana hiyo kabisa.
“Ibara ya 134 (2) ya Rasimu Inayopendekezwa
imeeleza kuwa idadi ya wabunge itakuwa kati ya 340 na 390 kwa kuzingatia
uwiano wa jinsia. Sasa kuzingatia ni kuzingatia tu, kama utazingatia
lakini hakuna mwanamke aliyejitokeza maana yake nini? Utasema
tumezingatia lakini hali ndiyo hiyo,” alisema.
“Katiba hii ilipaswa kueleza kwamba katika kila
jimbo kutakuwa na wagombea wanaume na wanawake watakaoshindana kuwania
uongozi, vinginevyo Katiba hiyo imeturudisha nyuma, tena unaweza kusema
afadhali ya Katiba ya mwaka 1977 kwa sababu ilisema kutakuwa na asilimia
30 ya uwakilishi wa wanawake bungeni.”
Hii si mara ya kwanza kwa Dk Kijo – Bisimba kutofautiana na mchakato mzima wa Katiba.
Katika hatua za awali, taasisi yake ilikuwa
ikifanya kazi kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu Katiba chini ya
kampeni yake ya Gogota na mara kadhaa alilaumu viongozi wa mikoa kwa
kukwamisha juhudi zao za kuelimisha wananchi kuhusu haki zao kwenye
nyaraka hiyo muhimu kwao na kuwahimisha kushiriki kikamilifu. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment