Idadi ya watu
waliolazwa hospitalini kwa kunywa togwa inayosadikiwa kuwa na sumu
katika Kijiji cha Litapwasi, Kata ya Mpitimbi mkoani Ruvuma imeongezeka
kutoka 270 hadi 340.
Tukio hilo lilitokea Jumapili baada ya watu
kushiriki sherehe ya Kipaimara ambako walikula, kunywa pombe na togwa na
baadaye wale waliokunywa togwa walianza kuumwa matumbo, kuhara na
kutapika.
Hadi jana, watu 102 walikuwa bado wamelazwa katika
Zahanati ya Lyangweni, Hospitali ya St. Joseph Peramiho na Hospitali ya
Mkoa wa Ruvuma.
Tayari watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa
upelelezi kuhusiana na tukio hilo, akiwamo Baba Mzazi wa mtoto Dickson
aliyepata kipaimara, Enes Nungu (47). Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela
aliwataja watu wengine wanaoshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi
Songea kwa mahojiano kuwa ni Benedict Nungu (76), Esebius Komba (36),
Sadiki Masodi (65) na John Kaulangudidi. Mtu anayedaiwa kukabidhiwa
ufunguo chumba cha vinywaji kabla ya kugawiwa kwa wananchi, Ridhiwani
Shawa haijulikani alipo.
Mabaki ya chakula, togwa na pombe ya kienyeji vilichukuliwa juzi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kamanda Mskhiela alitoa wito kwa wananchi
wanaoandaa sherehe kuhakikisha wanafanya hivyo katika mazingira mazuri
na yenye usalama ili kuepuka athari kama hizo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Peramiho, Dk Vanace
Mushi alisema hadi jana, watu waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo
walikuwa 34 na hakukuwa na mgonjwa aliyeruhusiwa kurudi nyumbani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa
Ruvuma, Majuto Mlawa alisema wagonjwa tisa wa rufaa walipokewa na
kupatiwa matibabu huku hali zao zikiwa mbaya.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,
Said Mwambungu alisema: “Jambo hili limenisikitisha sana, nimeumizwa
sana nawapa pole wote waliopatwa na tatizo hilo naamini Mwenyezi Mungu
atawasaidia na watapona na kurejea katika hali zao za kawaida.”
Hata hivyo, Mwambungu alisema hiyo ni ajali kama
nyingine, hivyo anaviachia vyombo vya usalama na wataalamu wa afya
kupata ukweli. Pia aliwataka wananchi kuwa makini pindi wanapoandaa
vyakula na pombe za kienyeji katika sherehe mbalimbali. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment