Friday, April 25, 2014

WANANCHI WANAUNGA MKONO RASIMU YA KATIBA


kigangwala2 7c529
Na Hudugu Ng'amilo.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya Twaweza umebainisha kuwa wananchi wanaunga mkono kwa kiwango kikubwa Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Ripoti ya utafiti huo uliofanyika Februari, mwaka huu kwa njia ya simu za mkononi na watu kuulizwa kuhusu mchakato wa Katiba, inaeleza kuwa kama wananchi wangeipigia kura rasimu hiyo mwezi huo, Katiba hiyo ingepitishwa kwa asilimia 65 Zanzibar na asilimia 62 Tanzania Bara.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi alisema kati ya watu waliohojiwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 20 wangepiga kura ya hapana, kwa upande wa Zanzibar watu ambao wangesema hapana wangekuwa asilimia 19.
"Watu ambao walisema hawana uhakika na hawajui lolote kwa upande wa Zanzibar ni asilimia 19 na Tanzania Bara asilimia 15," alisema.
"Zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walisema wana nia ya kupiga kura ya kuikubali Katiba (rasimu) kama ilivyo sasa."
Muundo wa Serikali
Kuhusu muundo wa Serikali, Mushi alisema: "Asilimia 80 ya Wazanzibari wanaunga mkono muundo wa serikali tatu. Kwa Tanzania Bara wanaounga mkono serikali tatu ni asilimia 43."
Alisema takwimu hizo ni tofauti na zilizotolewa miezi minane iliyopita ilipotolewa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, ambayo asilimia 51 ya wananchi wa Tanzania Bara walipendekeza muundo wa serikali tatu. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz

Alisema baada ya kutolewa kwa Rasimu mbili za Katiba (ya kwanza na ya pili), Wazanzibari wanataka uhuru zaidi wa kujitawala au muungano wa serikali tatu, huku wananchi kutoka Tanzania Bara wakigawanyika nusu kwa nusu juu ya muundo wa serikali wanaoutaka.
Mafuta na gesi
Kuhusu mafuta na gesi kutokuwa masuala ya muungano, bali chini ya mamlaka ya Serikali za Tanganyika na Zanzibar, Mushi alisema suala hilo lilikubaliwa na wananchi wa Tanzania Bara kwa asilimia 42 na Zanzibar asilimia 74.
Alisema Watanzania sita kati ya 10 (asilimia 60) wanaosikiliza mjadala kuhusu Rasimu ya Katiba, wanawaamini wabunge kuwa wanawakilisha masilahi yao bungeni, wanaunga mkono uwazi na uwajibikaji kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba.Mambo mengine ambayo yameungwa mkono na wananchi ni utaratibu wa kudhibiti na kuwawajibisha wabunge, uwepo wa mgombea binafsi na mgawanyo wa madaraka.
Utafiti huo umefanyika huku kukiwa na mvutano mkali katika Bunge Maalumu la Katiba kuhusu muundo wa muungano na kusababisha wajumbe wa Bunge hilo wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia kutokana na CCM kuunga mkono muundo wa serikali mbili ambao ni tofauti na Rasimu ya Katiba iliyopendekeza muundo wa serikali tatu.
Mushi alisema maoni ya wananchi ni muhimu yakazingatiwa bila kujali nini kinaamuriwa na wawakilishi kwenye Bunge la Katiba, kwa sababu baadaye watapiga kura ya maoni kupitisha Katiba.
Maoni ya kwanza ya utafiti huo yalikusanywa Tanzania Bara kati ya Februari 12 na Machi 4, mwaka huu na taasisi hiyo ilipata majibu ya kaya 1,547 na mengine yalikusanywa kati ya Julai 16 na Julai 30 mwaka jana na kaya 1,708 zilitoa majibu.
"Kwa upande wa Zanzibar, utafiti kwa kutumia simu ya mkononi ulifanyika Februari 24 na Machi Mosi, mwaka huu na kaya 445 zilitoa majibu," alisema.
CHANZO MWANANCHI.  
Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...