Meneja wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Mkoa wa Mbeya Rodney Alananga (picha na maktaba)
Na Mwandishi Wetu Wa Jambo Tz, Mbeya
LICHA ya Serikali kukataza uingizaji wa pombe haramu kutoka nchi jirani za Malawi na Zambia maarufu kama viroba hatimaye wananchi wamezidi kuziingiza pombe hizo na kutapakaa jijini Mbeya.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii Mkoani Mbeya umebaini kuwa pombe hizo zimekuwa zikiingizwa kwa njia za panya kupitia vivuko visivyohalali Wilayani Kyela na kusafirisha hadi jijini Mbeya ambako imeonekana kuwa ndiko kuna watumiaji wengi wa pombe hizo.
Katika wilaya ya Kyela wafanyabiashara wa pombe hizo wamekuwa wakisafirisha mithiri ya gunia la Mchele, juu yake wakiwa wamejaza maharage na wengine huweka dagaa za Nyasa ili vyombo husika visiweze kubaini kilichomo ndani yake.
Imebainika pia kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakipitisha pombe hizo katika Wilaya ya Ileje kwa kutumia Baiskeli na kuziingiza nchi kupitia eneo la Mbebe, Msia, Mapogolo, Ikumbilo, Bupigu, Ilondo na Ilulu.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Wakizungumza na Mwandishi wa habari baadhi ya wafanyabiashara wilayani Ileje wamesema kuwa biashara ya viroba kutoka nchi jirani za Malawi na Zambia inawalipa sana kutokana na bei zao kuwa ndogo licha ya kusafirisha kwa gharama ukilinganisha na viroba vya hapa nchini.
Wafanyabiashara hao ambao waliomba hifadhi ya majina yao wamesema kuwa mfuko wa viroba 300 wananunua kwa bei ya shilingi 40000 kwa bei ya jumla kutoka Malawi wakati wao wanauza kwa bei ya shilingi elfu 60000.
Hata hivyo walidai kuwa wakati mwingine wanauza kwa bei ya reja reja ambapo kiroba kimoja kinauzwa kwa bei ya shilingi 250 -300 jambo ambalo walisema kuwa inawanufaisha sana kuliko viroba vya hapa nchini.
Waliongeza kuwa viroba hivyo vimekuwa vikipendwa sana na watumiaji wakitanzania kutokana na bei zake kuwa ndogo ambapo walisema kuwa zinaendana na uchumi walionao kwani watumiaji hao hutumia gharama ndogo ukilinganisha na viroba vinavyotengenezwa nchini.
Walisema kuwa viroba vya hapa nchini vinauzwa kwa bei ghari ndiyo maana walio wengi hawapendi kuvitumia kwani kiroba kidogo kinauzwa kwa bei ya shilingi 600-700 wakati vikubwa vinauzwa kwa bei ya shilingi 1200-1500.
Aidha walisema kuwa viroba vya Bwenzi Charger, Raider, Boss na Power No 1 vikubwa vinauzwa kwa bei ya shilingi 400-500 jambo ambalo linawafanya watanzania wengi kukimbilia kuvinunua kuliko vya hapa nyumbani.
Akizungumzia kuhusu uingizwaji wa pombe hizo Meneja wa Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Mkoa wa Mbeya Rodney Alananga amesema kuwa kunachangamoto kubwa kuweza kuzuia uingizwaji wa pombe hizo nchini.
Alananga alisema kuwa suala la viroba linapaswa kushughulikiwa na wananchi kwa pamoja ili kuweza kutokomeza uingizwaji huo kwani kuachiavyombo husika haviwezi kutekeleza kwa muda mfupi.
Meneja huyo alisema kutokana na uhatari wa viroba hivyo kwa afya za watumiaji serikali ya Mkoa wa Mbeya imeunda kikosi maalumu kwa ajili ya kufanya operesheni kubwa ambapo kila atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema kuwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abass Kandolo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na Mamlaka husika wako katika hatua za mwisho kuanzakwa operesheni hiyo ya kukamata wale wote wanaouza viropba hivyo.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano na Mamlaka yake kwa kutoa taarifa wale wote wanaoingiza viroba kwa njia za magendo ikiwa ni pamoja na kutoa mianya inayotumika katika usafirishaji wa pombe hizo haramu.
Aidha alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa vivuko vingi Wilayani Kyela serikali inakusudia kusajiri vivuko hivyo ili kudhibiti uingizwaji holela wa pombe hizo pamoja na baadhi ya bidhaa nyingine kutoka nchi hizo.
Alisema kuwa viroba vingi kutoka nchi jirani za Malawi na Zambia havijathibitishwa na mamlaka husika kama vile TBS hivyo ni hatari kwa watumiaji kwani havina ubora wa viwango vinavyotakiwa kutumia.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
No comments:
Post a Comment