Saturday, December 28, 2013

LUMBESA LA VIPODOZI FEKI LAKAMATWA IRINGA


 Baadhi ya shehena za vipodozi  zilizokamatwa na jeshi la polisi mkoa wa Iringa baada ya kushushwa katika roli katika makao makuu makuu ya jeshi mkoa wa Iringa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi akionyesha shehena ya vipodozi vilivyokamatwa na jeshi hilo mkoani  Iringa katika makao makuu ya jeshi hilo jana. (Picha na Denis Mlowe)

JESHI la polisi mkoa wa Iringa limefanikiwa kukamata shehena ya vipodozi vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi iliyokuwa inasafirishwa kutoka nchini Zambia kwenda jijini Dar es Salaam vilivyopigwa marufuku kwa matumizi ya binadamu.


Shehena hizo zilikuwa zimebebwa na gari aina ya lori la mafuta lenye namba za usajili T 247 BHP na tela lenye namba usajili T 598 BMK mali ya World Oil Ltd ya jijini Dar es Salaam.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya vipodozi ni  Dereva wa lori Mohamed Sadru(23) na Kassimu Kaifa anayesadikika ndio mwenye mali.
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi  amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kusema kuwa walipata taarifa za kiitelejensia kutoka Tunduma kuwa kuna lori linasafirisha shehena hiyo kutoka nchini Zambia.
Mungi alisema walijiweka tayari kulikamata gari hilo kwa kukaa barabara kuu kuanzia saa moja jioni hadi ilipofika saa kumi alfajiri ndipo gari lilipofika na kukamatwa.
Anaongeza kuwa maafisa wa polisi mkoa wa Iringa walijipanga vizuri kuweza kulikagua gari hilo na waligundua kuna shehena kubwa ya vipodozi vilivyopigwa marufuku na TFDA na kuwaweka chini ya ulinzi dereva na roli hilo.


“Cha kushangaza gari la mafuta kuweza kubeba  vipodozi hivi vilivyopigwa marufuku hivyo tukaamua kuwashirikisha wadau wengine ambao ni TRA, TFDA na Tanroad kuweza kubaini makosa ambayo watuhumiwa hao wamefanya katika usafirishaji wa shehena hiyo.” Alisema Mungi
Mungi alisema uchunguzi wa awali unaonyesha shehena hiyo ina thamani kubwa na ndio maana watuhumiwa walikuwa wanasafirisha kwa njia ya magendo na wanaendelea kuchunguza kubaini thamani halisi ya mzigo huo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mamlaka wa Chakula na Dawa (TFDA) mkoa wa Iringa, Deodata Rukupwa alisema shehena iliyokamatwa asilimia 100 ina kemikali iliyopigwa marufuku ya Hydroqunone na mamlaka hiyo.


Alisema vipodozi hivyo vitateketezwa kwa pamoja na jeshi la polisi na gari hilo kutaifishwa na serikali kutokana na kubeba mzigo wa magendo.
Rukupwa aliwataka wananchi kuwa makini katika kutumia vipodozi vilivyopigwa marufuku na serikali na kutoa taarifa wanapobaini kuna vipodozi vilivyopigwa marufuku vinauzwa.
Source: Jiachie

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...