Wednesday, December 25, 2013

HILI NDILO BARAZA LA MAWAZIRI LINALOTAKIWA


Rais Kikwete. 
********
Baada ya kizaazaa cha wiki iliyopita ambapo mawaziri wanne walipoteza kazi zao kutokana na kuwajibishwa kwa vitendo vya ukatili na mauaji vilivyotokea wakati watendaji katika wizara zao walipokuwa wakiendesha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’ nchi nzima, kinachosubiriwa na wananchi hivi sasa ni Rais Jakaya Kikwete kuunda Baraza jipya la Mawaziri.
Kutokana na udhaifu mkubwa katika utendaji ambao kwa muda mrefu umeonyeshwa na mawaziri wengi katika Baraza la Mawaziri, hatudhani kama kuna mwananchi hata mmoja  anayemtarajia Rais Kikwete kujaza tu nafasi za mawaziri aliowafukuza wiki iliyopita.
Nderemo na vifijo vilivyotokana na furaha ya wananchi katika kila kona ya nchi baada ya mawaziri hao kuondolewa katika nyadhifa zao ni ishara tosha kwamba hawamtarajii Rais Kikwete kuishia hapo, isipokuwa kuwaondoa mawaziri wengine wengi ambao tayari wamethibitika na hata kutajwa na chama chao cha CCM kuwa ni ‘mawaziri mizigo’.

Hii bila shaka ni fursa nzuri kwa Rais Kikwete kusoma alama za nyakati, kwamba wananchi wamefika kikomo cha uvumilivu na sasa wamechoka na uzembe unaotokana na mawaziri dhaifu walio katika Baraza lake la Mawaziri. Hao ni  mawaziri ambao karibu muda wote wamekuwa nyuma ya matukio na kuishia kuwa watazamaji, huku shughuli za Serikali zikienda ndivyo sivyo kutokana na kutochukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, ubadhirifu wa fedha za umma na ufisadi uliokithiri.
Kutokana na mawaziri wengi kutokuwa na dhamira wala uwezo wa kuthubutu na kutenda, programu za Serikali kama ‘Kilimo Kwanza’ na ‘Matokeo Makubwa Sasa’ zimebakia kuwa vichekesho vya karne, pamoja na kuanzishwa kwa mbwembwe na fedha nyingi za walipakodi.
Ni bahati mbaya kwamba Rais Kikwete amebaki na muda mfupi mno kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi Oktoba 2015. Kwa kifupi, amebakiwa na miezi 22. Kutokana na kuwapo programu nyingi ambazo hazijatekelezwa, anahitaji sasa kujipanga upya na kupata Baraza jipya la Mawaziri lenye watendaji waadilifu na wachapakazi. 
Baadhi ya wananchi wamekuwa wakielekeza lawama nyingi kwake kwamba uteuzi wake wa mawaziri kwa kiasi kikubwa umekuwa siyo wa umakini kwa maelezo kuwa, hauzingatii vigezo vya ufanisi na utumishi wa umma uliotukuka. Kwamba wengi wamekuwa ni mawaziri wa kufunga tai na kupeperusha bendera kwenye ‘mashangingi’ yao.
Tunakubaliana na wanaosema kwamba mawaziri wachapakazi katika Baraza lake wanahesabika katika kiganja cha mkono na kwamba Baraza hilo ni kubwa mno kupita kiasi. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni mawaziri wasiozidi saba  wanaoweza kusimama leo na kuonyesha kitu walichokifanya na kukisimamia mpaka mwisho. Rais Kikwete atafanya vyema iwapo ataweka mfumo wa kupima utendaji wa mawaziri wake na kuwawajibisha wale wasiofikia viwango, badala ya kusubiri shinikizo la Bunge kama tulivyoshuhudia mwishoni mwa wiki.
Tunamshauri Rais Kikwete sasa aepuke kigezo cha ukanda na ukabila katika kuteua Baraza la Mawaziri. Hoja yetu ni kwamba siyo lazima kila kanda au mkoa kuwakilishwa na idadi sawa ya mawaziri hata kama baadhi yao hawana uwezo hata kidogo. Tunasema vigezo vikubwa katika uteuzi huo viwe ni uzalendo, uadilifu na utendaji, hata kama vigezo hivyo vitalazimu kuteuliwa mawaziri wawili kutoka katika kitongoji, kijiji au kata moja.
MWANANCHI

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...