Friday, December 27, 2013

HII HAPA NDIO SIRI YA PINDA KUNUSURIKA

*Katibu Umoja wa Wanawake aadhirika kikaoni
*Wabunge 178 waomba kikao na Kinana

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
KATIKA hali isiyo ya kawaida, Ijumaa iliyopita Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliponea chupuchupu kung’olewa uenyekiti wa kikao cha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kikao hicho (party caucus) kilifanyika baada ya hali ya hewa bungeni kuchafuka baada ya kuwekwa hadharani bungeni ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyosomwa na Mwenyekiti wake James Lembeli.

Ripoti hiyo ilihusu tathmini ya upungufu kadha wa kadha uliojitokeza wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, upungufu ulioibua mjadala mzito bungeni, na kusababisha mawaziri wanne kujiuzulu.

Mawaziri hao ni Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na David David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi). Hata hivyo habari zilizopatikana zilisema mawaziri hao waling’olewa kwa amri ya Rais Jakaya Kikwete.

Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like ukurasa wetu wa facebook bofya neno  Jambo Tz
Taarifa za ndani kutoka kwenye kikao hicho zilisema kuwa, Mbunge wa Jimbo la Sikonge Said Nkumba ndiye aliyewasha moto dhidi ya Pinda kwa kumtaka ajiondoe kwenye nafasi ya uenyekiti wa kikao hicho.

“Kwenye kikao chetu hali haikuwa nzuri, Mheshimiwa Nkumba alimtaka Waziri Mkuu ambaye kikanuni ndiye Mwenyekiti wa kikao ajiondoe mwenyewe kwenye uenyekiti kutokana na udhaifu wake kiutendaji.

“Na kweli bwana, baada ya Nkumba kumbana Pinda kweli kweli, tukashangaa kumuona Waziri Mkuu akielekea kutekeleza yale yaliyosemwa na Nkumba, lilikuwa jambo la kustaajabisha sana.

“Lakini kabla hajatekeleza matakwa ya Nkumba na wabunge wengine, akasimama Mbunge wa Mtera Job Lusinde na kumtaka Waziri Mkuu aendelee na uenyekiti wa kikao chetu, kwa sababu kama angetoka kama alivyotaka kufanya, basi ungekuwa mwanzo wa mwisho wake,” kilisema chanzo chetu.

Taarifa zilisema kuwa, baadhi ya wabunge walilumbana kwa kiasi kikubwa huku baadhi yao wakimtetea Waziri Mkuu wakidai mfumo uliopo unamfanya kushindwa kuchukua hatua ikiwamo ya kuwafukuza kazi watendaji waandamizi serikalini, huku wengine wakitaka ang’oke kutokana na udhaifu wake kiutendaji.

Katika kikao hicho, wabunge wa CCM walisimamia hoja ya kuwataka mawaziri waliotajwa kwenye ripoti ya Lembeli wajiuzulu.

Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo saa 2:09 usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo.

Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “Mimi ni mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge. Rais Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake, yaliyotokea yametokea lakini hali ya wanyama huko si nzuri”

“Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa hii kuachia ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida kuijulisha sehemu inayohusika(Rais).

Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo hawakuwapo ndipo alipoitwa Dk. Mathayo na kutoa maelezo yake.

Katika maelezo yake Dk. Mathayo alisema kuwa ripoti hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumuhoji na kwamba hata ripoti nzima haikueleza yeye kuhusika na kashfa hiyo.

Hata hivyo akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk. Mathayo ameshindwa kusimamia mapendekezo tisa, yakiwamo matatizo ya wafugaji aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.

Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute Mkuu wa nchi (Rais Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali ushauri wa Bunge; amekubali kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wao(mawaziri).”
MTANZANIA
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like ukurasa wetu wa facebook bofya neno  Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...