Sunday, November 24, 2013

LOWASSA AIELEZEA ILANI IJAYO YA CCM


Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli Mh. Edward Lowassa akiwahutubia wakazi wa Kigamboni.
******
Waziri mkuu mstaafu na mbunge wa Monduli Mh. Edward Lowassa amewaomba wanachama wa CCM kushawishi suala la elimu bure na bora liwe ajenda ya kwanza katika Ilani ijayo ya uchaguzi ya Chama hicho.
Akiwahutubia wananchi wa kata ya Kigamboni ambako alikuwa mgeni rasmi katika sherehe ya kukabidhiwa madawati shule za msingi za kata hiyo, Mh Lowassa amesema kwa maoni yake anapendekeza suala hilo liwe ajenda ya kwanza katika Ilani ya uchaguzi ya ccm.
"Wana CCM wenzangu naomba tushawishi suala la elimu bure kwa wanafunzi wote wa shule tena elimu bora liwe la kwanza katika ilani ijayo ya uchaguzi" alisema Lowassa na kushangaliwa na mamia ya wananchi wa kata hiyo.
Alisema kuwa ana ndoto hiyo kuwa siku moja elimu itakuwa bure tena elimu iliyo bora, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kujenga usawa wa matabaka kwa taifa letu.
Lowassa ambaye ni miongoni mwa wana CCMinakosemekana yuko katika mbio za kuwania urais uchaguzi ujayo, alisema kuwa kutokana na hali nzuri ya uchumi hivi sasa suala hilo linawezekana.
"Wakati Mzee Mkapa anaingia alikuta madeni mengi sana Serikali yake ikafanya juhudi kulipa na kuanza kukopesheka, Rais Kikwete yeye ameunyanyua uchumi kwa kuimarisha miundo mbinu na sasa hali ni nzuri kabisa, hebu sasa tuelekeze nguvu katika elimu"alisema na kuongeza iwe kipaumbele cha sasa.
Ametoa changamoto kwa wale wanaingana na fikra zake za kutaka elimu bure na bora, wajenge hoja katika mitandao na si kupinga tu."Najua wako watakaobisha na kusema sana katika mitandao, lakini mimi nawaomba wabi she kwa hoja na uwe ni mjadala katika mitandao na si kupinga tu, haisaidii" alisema Lowassa na kuongeza ni mbaya sana kuona wanafunzi wanakaa chini wakati uwezo wa kuboresha hali hiyo pamoja na maslahi ya waalimu upo.
Katika kuonesha kuguswa na watoto wa shule za msingi za kata hiyo kukaa chini, Mh Lowassa alisema anachangia madawati 100, na kutoa changamoto kwa wadau wengine wa elimu kusaidia zaidi. 
Pia aliahidi kuchangia shillingi milioni 10 kwa kikundi cha vicoba Cha kina mama Kigamboni ambao wamemuomba mke wa Mh Lowassa mama Regina kuwa mlezi wao.Lowassa alisema atajaribu kumshawishi mke wake akubali jukumu hilo.
Aidha akijibu risala ya wananchi wa Kigamboni waliyomuomba kusaidia kujua hatma ya mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Kigamboni, Lowassa alisema anaamini suala hilo linashughulikiwa vilivyo na waziri wa adhi na makazi Profesa Anna Tibaijuka kwani ni msomi mzuri ana uzoefu wa kimataifa na masuala hayo na zaidi ni mchapa kazi hodari.
Sherehe hizo zilikuwa ni za kukabidhiwa kwa madawati 100 kwa shule 4 za msingi zilizopo katika kata hiyo ya Kigamboni, ambayo yametolewa na diwani wa kata hiyo Dotto Msawa

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...