Wednesday, August 28, 2013

KODI YA SIMU BADO KIMBEMBE...!!!


                       Waziri wa Fedha, William Mgimwa

Wakati wananchi wakiwa hawajajua majaliwa yao juu maamuzi ya serikali kuhusu kilio chao dhidi ya kodi ya simu ya Sh. 1,000 kwa mwezi iliyopitishwa na Bunge la Bajeti ya mwaka 2013/14, kuna habari kwamba mzigo huo sasa unaweza kuhamishiwa kwenye ununuaji wa vocha.
Hofu hii inajengeka wakati Mkutano wa Bunge wa 11 ambao unatarajiwa kujadili suala la kodi ya simu ukianza mjini Dodoma huku kukiwa na habari kwamba serikali inatafakari uwezekano wa kupandisha ushuru kwenye vocha (excise duty) kwa asilimia 5.5.
Kama maamuzi hayo yatafikiwa ushuru huo utapaa hadi kufikia asilimia 20 kutoka asilimia 14.5 wa sasa.
Mpango huo wa serikali ni moja ya mikakati yake ya kuziba pengo la kiasi cha Sh. bilioni 178.5 kama kodi ya simu itaondolewa kwani ilikuwa imekadiriwa kuwa ingeingiza mapato ya kiwango hicho kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
 
Kama ushuru huo utaongezwa na kukubaliwa na wabunge, basi Tanzania itakuwa na ushuru mkubwa kwenye simu kuliko viwango vinavyotozwa na nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

 
Rwanda inaelezwa kuwa na viwango vya chini kabisa vya ushuru huo wa asilimia nane, Kenya asilimia 10 wakati Uganda ni asilimia 12.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari toka serikalini, ongezeko la kiwango hicho kipya cha ushuru, ni matokeo ya kazi ya kikosi kazi kilichoundwa na Waziri wa Fedha na kuwashirikisha wajumbe sita kutoka serikalini na wadau wengine  wakiwamo Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Simu za Mkononi (MOAT).
 
Kikosi kazi hicho kiliundwa ili kujadili njia nzuri ya kutoza ushuru wa laini za kadi, uliopitishwa na Bunge katika kikao chake cha bajeti kilichofanyika Aprili hadi Julai mwaka huu.
KAULI YA WAZIRI WA FEDHA
Hata hivyo, jana NIPASHE lilipomuuliza Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kuhusiana na uamuzi mpya wa serikali, alisema mwafaka kuhusiana na suala la kodi ya simu utajulikana baada ya kumalizika kwa majadiliano ya kikosi kazi ambayo alisema kuwa yanaendelea.
 
 “Unasema kuna taarifa kwamba serikali inakusudia kuhamishia kodi ya simu kwenda katika vocha, lakini nataka kukuambia kwamba suala la kodi ya simu lipo katika majadiliano, hayo ndiyo yatakuja na maamuzi sahihi juu ya suala hilo,” alisema Dk. Mgimwa na kuongeza:
“Majadiliano hayo yanatarajia kukamilika muda siyo mrefu, hivyo msubiri tutatoa taarifa kamili.”
Tembelea http://jambotz8.blogspot.com/ kila siku.
 
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2013/14 bungeni Juni 13, mwaka huu, Waziri Mgimwa alitangaza kuanzishwa kwa kodi mpya ya laini za simu ambayo ilitarajiwa kuanza kutozwa Julai Mosi, mwaka huu.
 
Dk. Mgimwa alisema kuwa, chanzo hicho kipya cha mapato ya serikal, kilikuwa kinakusudia kutoza ushuru kwenye huduma zote za simu za mkononi badala ya muda wa maongezi peke yake.
Alifafanua kuwa asilimia 2.5 ya mapato ya kodi hiyo yalitarajiwa kugharimia elimu nchini kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati Maalum ya Spika ya Kushauri kuhusu mapato na matumizi ya serikali.
Hata hivyo, kodi hiyo ilipingwa kwa nguvu na  wananchi, taasisi na baadhi ya kampuni za simu nchini, vyama vya siasa kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chenye serikali iliyoko madarakani.
 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia wabunge wake wawili, John Mnyika (Ubungo) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), walikuwa mstari wa mbele kupinga kodi hiyo, kwa kuonyesha jinsi itakavyoumiza wananchi.
 
Mnyika alikusanya saini za wananchi 26,000 wanaopinga mpango huo wa serikali ili awasilishe bungeni hoja ya wananchi kupinga tozo hiyo.
Hadi sasa ameshakusanya zaini ya saini 26,000.Kwa upande wake, Zitto alisema kodi hiyo haikujadiliwa kabisa kwa kuwa iliondolewa katika mapendekezo ya mapato, lakini ikarejeshwa kupitia Muswada wa Fedha ambao hutafsiri hotuba ya bajeti kisheria.
 
Hali kadhalika, Rais Jakaya Kikwete, alikaririwa akisema kuwa muswada wa sheria ya fedha kuhusu kodi za laini za simu, utarejeshwa tena katika mkutano wa Bunge wa sasa kujadiliwa upya. 
Tembelea http://jambotz8.blogspot.com/ kila siku.
 
Rais alitoa kauli hiyo alipokutana na wadau wa Taasisi ya Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) wakati wa chakula cha jioni jijini Dar es Salaam Agosti 16, mwaka huu.
Serikali inalalamikiwa kukimbilia kutoza kodi kubwa katika simu kwa watumiaji wa huduma hizo na kusahau kwamba simu siyo anasa bali ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi kwa kuwa ni chanzo cha kupata taarifa mbalimbali na pia zinarahisisha uhamishaji wa fedha.
Kilio cha wengi ni kutaka kampuni za simu ambazo zinatengeneza faida kubwa kutozwa kodi hiyo badala ya watumiaji kwa kuwa zimekuwa zikiwatoza gharama watumiaji hata kama hawakupata huduma. 
jambotz8.blogspot.com
Aidha, kampuni za simu zinalalamikiwa kwamba mapato yake ni vigumu kujulikana kwa mamlaka mbalimbali za serikali zikiwamo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika hatua nyingine, ratiba ya Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano unaoanza leo haionyeshi kama suala la kodi katika laini za simu litajadiliwa kama ilivyoahidiwa na Dk. Mgimwa wiki kadhaa zilizopita.
 
Hata hivyo, Dk. Mgimwa jana alilieleza gazeti hili kuwa huenda suala hilo likawekwa katika ratiba ya vikao vya Bunge itakayotolewa leo.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Elizabeth Zaya, Dar na Boniface Luhanga, Dodoma.

SOURCE: NIPASHE

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...