Akizungumza
na waandishi wa habari janaMkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba amesema kitendo cha
Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu matumizi ya nguvu kwa polisi dhidi
ya raia ni cha kulaaniwa na wapenda haki wote na amemtaka waziri mkuu
kuwaomba radhi watanzania.
KUPINGA KAULI YA WAZIRI MKUU "Wapigwe tu" ALIYOITOA BUNGENI TAREHE 20/06/2013
Taarifa
hii ni matokeo ya ufuatiliaji wa utendaji wa shughuli za Serikali kama
zinavyowasilishwa bungeni na kauli ya Waziri Mkuu (Mtendaji Mkuu wa
shughuli za serikali Bungeni) aliyoitoa, Alhamisi ya tarehe 20 Juni
2013, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo. Waziri Mkuu Pinda,
alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama, hususan Jeshi la Polisi
kuwapiga wananchi watakao kaidi na kupinga amri halali ya jeshi hilo.
Katika tamko hilo, Pinda alisema Serikali imechoshwa na vurugu na
kwamba hakuna namna nyingine ya kupambana na wananchi wanaodharau vyombo
vya dola zaidi ya kipigo.
Waziri Mkuu Pinda alitoa msimamo huo
Bungeni, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza
Mangungu (CCM), aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali
kufuatia kuwa na matukio ya vurugu ya mara kwa mara nchini, hususan
huko Mtwara na Arusha.
Katika majibu yake, Mh. Pinda, pamoja na mambo
mengine alisema kuwa; “Mheshimiwa Mangungu hapa ameanza vizuri, lakini
mwisho hapa naona anasema vyombo vya dola vinapiga watu, ukifanya fujo
au umeambiwa usifanye hiki ukaamua kukaidi utapigwa tu. Akaendelea
kusema kuwa, “Lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa
misingi ya sheria na kama wewe umekaidi, unaona kwamba ni imara zaidi,
wewe ndio jeuri zaidi, watakupiga tu.
“Na
mimi nasema wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi muwapige tu, kwa
sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na wakaidi zaidi ya
kuwapiga,” alisema Pinda.
Ndugu wanahabari, Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu kimepokea kwa mshituko kauli hii iliyotolewa
na kiongozi wa juu serikalini. Maudhui ya kauli hii ni kinyume kabisa
cha Katiba ,Sheria za nchi na misingi ya haki za binadamu. katika miaka
ya hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za
binadamu hasa yale yanayotokana na vyombo vya dola na jeshi la polisi
nchini, ambapo jeshi la polisi limekuwa likitumia nguvu kubwa kupita
kiasi katika matukio mbali mbali na kusababisha vifo na kujeruhi watu
na hata watu ambao hawakukiuka amri halali ya jeshi hilo.
Matukio
haya ya matumizi makubwa ya nguvu za dola ni kinyume na taratibu za
utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 13
(1) Usawa mbele ya sheria , (3)” Haki za raia, wajibu na maslahi ya
kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na
vyombo vingine vya mamlaka ya nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu
wa sheria” na (6) (b) ambayo inasema ni “Ni marufuku kwa mtu
………….kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka atakapo thibitika kuwa
anayohatia ya kutenda kosa hilo” (e) Ni marufuku kwa mtu kuteswa,
kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazo mtweza au kumdhalilisha.”
Pia
ni Kinyume na kifungu namba 21 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai inayounda sura namba 20 ya sheria za Tanzania inayozuia matumizi
ya nguvu kupita kiasi na kifungu namba 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi
na Huduma saidizi “Police force and auxiliary Act” Sura namba 322 kama
zilivyorekebishwa mwaka 2002, ambayo inaelekeza kukamatwa kwa mtu
aliyetenda kosa na si kupigwa. Matumizi makubwa ya nguvu pia ni kinyume
na Mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania na inayotambuliwa
kwenye Katiba kama Tamko la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 na Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa Mwaka 1966.
Tungependa
kumkumbusha mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa Utawala wa sheria unajumuisha
serikali, na vyombo vya utekelezaji na ulinzi pamoja na wananchi
kuheshimu sheria. Na sio kuvunja sheria kwa vyombo vya usimamizi wa
sheria. Tamko hili la Waziri Mkuu limetoa mwanya mkubwa na a nguvu kwa
vyombo vya usimamizi wa sheria kuvunja haki za raia. Ikumbwe kuwa yapo
matukio mengi ya polisi kutumia vibaya nafasi yao na nguvu waliyonayo
katika kuwavunjia haki wananchi kama mauaji yaliyofanywa huko Songea
mwezi wa Pili mwaka 2012 ambapo watu wawili waliuwawa na polisi na
wengine 48 kujeruhiwa, Iringa mwezi wa tisa 2012 ambapo mtu mmoja
aliuwawa (Daudi Mwangosya), Tabora - Usinge 2011 ambapo mtu mmoja
aliuwawa. Haya ni baadhi tu ya matokeo ya matumizi makubwa ya nguvu ya
polisi. Pamoja na hayo yapo matukio ya polisi kuuwa raia na kuwajeruhi
kwenye matukio tofauti tofauti hapa nchini ambayo mpaka sasa Kituo kina
matukio ya watu 11 ambao wameuwawa mikononi mwa polisi. Haya yote
yanatokea kwa sababu jeshi la polisi limeshindwa kufanya kazi zake kwa
kuzingatia sheria na pia kutambua wajibu wao kwa wananchi.
Katika
hali hii ya kushtusha, kwenye nchi yenye Amani na Utulivu na kama
tunavyopenda kusema kisiwa cha amani, kiongozi huyu wa ngazi za juu
anatoa tamko linaloashiria kutoa ruksa kwa Jeshi la polisi kuvunja
sheria tena tamko linatolewa hadharani, mbele ya chombo kinachoheshimika
kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tofauti na misingi ya
Katiba na Haki za Binadamu ni hatari kwa amani na utulivi huo. . Waziri
Mkuu anapaswa kuheshimu na kuilinda katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania na Sheria za nchi na kuhakikisha usalama wa raia.
Hivyo
basi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na
Watanzania wanaopenda heshima ya sheria na haki za binadamu na asasi za
kiraia tumeendaa waraka unaokusanya saini za watanzania zikimtaka
Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda;
1. Kwanza kabisa kufuta kauli yake aliyoitoa bungeni kubariki polisi kupiga raia katika Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.
2. Kuwaomba radhi Watanzania kwa kile alichosema bungeni.
3.
Kulielekeza jeshi la polisi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na
taratibu zilizoko katika kutekeleza kazi zake za kulinda usalama wa raia
na mali zao.
Mpaka sasa tumeshakusanya saini 1000 kudai kauli hii ifutwe ilikulinda maisha ya Watanzania.
No comments:
Post a Comment