Wednesday, June 19, 2013

CCM YAOMBWA IRUHUSU WATU KUJITANGAZA URAIS.

VUGUVUGU la Uchaguzi Mkuu wa 2015 linazidi kupamba moto ambapo juzi aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, ameomba CCM itoe ruhusa mapema kwa wanaowania urais kuanza kutangaza nia lakini bila kukampeni.

Sumaye ambaye alipata kugombea urais mwaka 2005, alionya kuwa kama CCM haitaruhusu wagombea kutangaza nia leo, yanayofanyika chini chini ni mabaya zaidi.

Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 juzi, Sumaye mbali na kuitaka CCM kuruhusu wanachama wake kuan

za kutangaza nia ya kugombea mapema, pia alielezea athari za muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Rasimu ya Katiba mpya na mfumo mpya wa kusoma Bajeti ya Serikali bungeni.


Urais 2015


“Mimi Sumaye nikisema sasa nitagombea urais mwaka 2015 hakuna ubaya kwa kuwa Watanzania, watapata muda kunichambua na mpaka miaka miwili ikifika wakati wa kugombea, watakuwa wananifahamu,” alisema Sumaye.

Alihadharisha kuwa kama CCM itaendelea kukataza watu kutangaza nia mapema, wataanza kupita chini chini na madhara yake ni makubwa kuliko kuanza kutangaza nia mapema.

Kwa mujibu wa Sumaye, alisoma katika vyombo vya habari vikimkariri Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiruhusu wanaotaka kugombea urais, waanze kujitangaza lakini wasifanye vurugu, akaona ni hatua nzuri.
Lakini muda mfupi baadaye, alisoma vyombo vya habari vikimkariri Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, akisema watakaoanza kujitangaza chama kitawaengua.

“Sasa sina hakika na taarifa hizi za vyombo vya habari kwa kuwa katika matamshi hayo yote mimi sikuwepo... natii msimamo wa chama changu, ingawa binafsi nadhani ni vema tutangaze mapema lakini tusifanye kampeni,” alisema.

Katiba ya mapambano
Akizungumzia Rasimu ya Katiba mpya, Sumaye alisema mapendekezo ya Serikali tatu katika Rasimu hiyo, hata yeye aliona mapema kuwa hayaepukiki, lakini athari yake ni kujenga mapambano makubwa kati ya serikali hizo.

Alipendekeza wakati wa kujadili Rasimu, Watanzania watoe maoni ya namna ya kupunguza mapambano hayo ambayo yanaweza kuwa magumu kuliko wakati huu wa serikali mbili.

Alitoa mfano wa mapambano yaliyopo wakati huu wa serikali mbili kwamba yalisababisha Zanzibar ikaanza kudai Wimbo wa Taifa, Rais wa Zanzibar kupigiwa mizinga ambayo ilianza 19, sasa ni 21.

Mapambano mengine ni Zanzibar kudai kuwa Tanzania Bara inafaidika kwa kuwa Rais wa Jamhuri anasimamia mambo ya Muungano na ya Bara, wakati Bara inaona Muungano unaibeba Zanzibar.

“Kama mapambano haya hatujayaondoa wakati huu wa serikali mbili, katika serikali tatu mapambano ya Zanzibar na Bara ambayo watu wanaweza kuiita Tanganyika, yatakuwa makubwa zaidi na pengine mabaya,” alisema Sumaye.

Katika mfumo wa serikali tatu, Sumaye alihadharisha kwamba mapambano yataanzia katika mgawanyo wa rasilimali, wakati wa kugawa kodi za Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Bara.

Alihadharisha kuwa kuna uwezekano wa kutokea mapambano kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Tanzania Bara katika mgawanyo wa rasilimali na akaongeza kwamba kwa kuwa Serikali hizo mbili hazitakuwa na tofauti kubwa, mapambano hayo yatakuwa mabaya.

Mapambano mengine alisema yataanzia katika madaraka, ambayo alitoa mfano wa madai ya Zanzibar ya wakati wa serikali mbili, kwamba wakati wa serikali tatu, Bara nayo italeta madai yake.

Katika utendaji, Sumaye alisema pia kutakuwa na mapambano, kwa kuwa kutakuwa na marais watatu, makatibu wakuu viongozi watatu na makatibu wakuu wengine.

“Kwa sasa makatibu wakuu hawaingiliani, lakini katika serikali tatu, watavutana,” alihadharisha. Utaratibu mpya wa Bajeti Akizungumzia utaratibu mpya wa bajeti ya Serikali ambao wabunge wanaanza kujadili bajeti za wizara na kumaliza na Bajeti ya Serikali, Sumaye alisema utaratibu huo ni mbovu.

Kwa mujibu wa Sumaye, kwa utaratibu wa sasa Waziri akibanwa, atakubali kuongeza bajeti na hivyo atalazimika kurudi kwa wananchi, kutoza kodi zaidi ili apate hizo fedha.

Alisifu utaratibu wa zamani wa kuanza na Bajeti ya Serikali, kwa kuwa ilizuia bajeti kuvurugwa na wabunge walikuwa na fursa ya kubadili mafungu tu na si kuongeza bajeti.

“Kwa sasa wabunge wanaweza kutaka fedha nje ya mfuko wa bajeti, sasa Serikali ifanyeje? Waziri ataongeza kodi mpaka atamwumiza mlipa kodi,” alisema Sumaye.
CHANZO HABARILEO.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...