Waziri
wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akizindua
kitabu cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa
wa Morogoro Mhe. Saidi Amani na kushoto ni Eng. Joseph Nyamuhanga,
Mkurugenzi wa Barabara katika Wizara ya Ujenzi.
Msajili
wa Bodi ya Wabunifu na Wakadiriaji Majenzi, Arch. Jehad akipokea kitabu
cha Mwongozo wa Usanifu wa Barabara kutoka kwa Waziri wa Ujenzi,
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) mara baada ya kuzinduliwa
rasmi. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Saidi Amani.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert E. Mrango akipokea kitabu cha
Mwongozo wa Usanifu wa Barabara kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli, mara baada ya kuzinduliwa rasmi.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Eliya Ntandu akipokea kitabu cha Mwongozo
wa Usanifu wa Barabara kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli (katikati) mara baada ya kuzinduliwa rasmi. Kulia ni
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Saidi Amani.
Waziri
wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (wanne kutoka kushoto)
akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa
Wizara ya Ujenzi na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Morogoro.
Waziri
wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (Mb), leo amezindua
Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi ambalo linakutana kwa siku
mbili mjini Morogoro. Wakati akiongea katika uzinduzi wa Baraza hilo
linalojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara
ya Ujenzi, Mheshimiwa Magufuli amewapongeza watendaji wakuu wa wizara
na taasisi zake kwa namna wanavyosimamia utekelezaji wa majukumu yao kwa
ufanisi. “Mafanikio yanayoonekana kupatikana kwa upande wa wizara yetu
ni matokeo ya usimamizi wenu mzuri” alielezea Waziri Magufuli na
kuwataka kutorudi nyuma kwani hiyo ni dhamana waliyopewa na Taifa.
Akizungumzia
changamoto zilizopo, Waziri Magufuli alisisitiza kukerwa kwa kuendelea
kujitokeza vitendo vya rushwa katika vituo vya mizani na kwenye vivuko.
Mhe. Magufuli amezipongeza hatua zilizokwisha kuchukuliwa na Mtendaji
Mkuu wa Tanroads kwa kutangaza ajira za wafanyakazi wa vituo vya mizani
na amemtaka kukamilisha mapema ajira za Wahandisi watakaosimamia vituo
hivyo. “Hatua hizi tuzimechukua baada ya kubaini kuwa karibu asilimia
themanini ya watendaji waliopo katika vituo vya mizani ni wala rushwa”
alibainisha Mheshimiwa Waziri Magufuli.
Kwa
upande mwingine Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nao umepewa siku
sitini ili kuanza zoezi la ukatishaji tiketi za elektoniki hasa katika
kivuko cha Kuvukoni jijini Dar es Salaam. Waziri Magufuli alibainisha
baadhi ya mbinu zinazotumiwa na watendaji wasio waaminifu katika vivuko
hivyo, kuwa ni pamoja na kujichapishia tiketi kwa siri na wakati
mwingine kutochana tiketi wanazozipokea kutoka kwa abiria kwa lengo la
kuziuza tena.
Waziri
Magufuli hata hivyo amepongeza zoezi la kukamata magari ya Serikali
yanayotumia namba za binafsi kinyume na sheria. “Tayari hadi sasa jumla
ya magari 1,830 tayari yamekamatwa na kusajiliwa kwa namba za Serikali”
alifafanua Mheshimiwa Magufuli..
Wakati
huo huo Waziri wa Magufuli pia amekizundua Kitabu cha Mwongozo wa
Usanifu wa Barabara. Kitabu hicho kitatumiwa katika utekelezaji wa
shughuli za ujenzi na matengenezo ya barabara hapa nchini.
Wakati
akizindua kitabu hicho Mheshimiwa Waziri amewapongeza Mameneja wa
Tanroads wa mikoa ya Dodoma na Morogoro kwa ubunifu ambao wameuonyesha
kwa kutumia fedha wanazotengewa katika bajeti zao. Alielezea
kufurahishwa na kazi za upanuzi wa barabara unaoendelea kuanzia eneo la
Ihumwa hadi Dodoma Mjini ambao ni matokeo ya jitihada za watendaji
wenyewe mkoani. Hapa Morogoro pia kazi hizi za upanizi wa barabara
zimeelezwa kuanza kutekelezwa wakati ambapo mkoani Tabora tayari kuna
zaidi ya kilometa sita za lami zimejengwa kwa kutumia fedha zilizotengwa
katika bajeti ya mkoa. “Ninawaelekeza Mameneja wa Tanroads katika mikoa
mingine nanyi muwe na ubunifu na sio kukaa bila ya kuchukua hatua
zozote hata pale ambapo tayari kuna bajeti iliyopitishwa” alimalizia
Mheshimiwa Magufuli.
No comments:
Post a Comment