Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (katikati) akiwa na walinzi wake
akiwasili katika Jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam, jana kushiriki
kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho. Picha na Michael Jamson
********
Hali ya wasiwasi iligubika eneo kinapofanyika kikao cha Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichoanza Dar es
Salaam jana.
Ulinzi mkali wa walinzi wa Chadema (Blue Guard),
uliimarishwa katika ukumbi wa Ubungo Plaza kinapofanyika kikao hicho
ambacho kinatarajiwa kumalizika leo, huku kukiwa na maagizo
yaliyoashiria kuwapo kwa mambo mazito.
Maazimio ya kikao hicho yanasubiriwa kwa hamu na
wafuatiliaji wa mambo ya siasa nchini kwani kinafanyika katika kipindi
ambacho chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapita katika misukosuko
na hasa ya malumbano baina ya makamanda wake wa juu.
























