Amina Mohamed,waziri wa mambo ya nje wa Kenya
Kenya imekuwa nchi ya kwanza kutoka
Jumuia ya Afrika Mashariki kuipongeza Tanzania kwa hatua yake ya
kutangaza bayana kwamba haiko tayari kutoka katika jumuiya hiyo kama
ilivyodhaniwa.
Wasiwasi kuwa Tanzania ingejitoa
kutoka jumuia ya Afrika Mashariki ulitokana na hali iliyojitokeza kwa
baadhi ya nchi za jumuia hiyo kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha
Tanzania na Burundi.
Baadhi ya wanasiasa na wananchi nchini
Tanzania walitaka nchi yao iachane na jumuia hiyo wakizishutumu Kenya,
Rwanda na Uganda kuitenga Tanzania hata katika mikutano ya masuala
yaliyohitaji maamuzi ya jumuia.
Kufuatia mfarakano huo, ulionekana
kutishia uhai wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete wa
Tanzania, wiki hii alilihutubia bunge la Muungano wa Tanzania mjini
Dodoma, katikati ya nchi na kutangaza bayana kuwa Tanzania haitatoka
katika jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani imefanya kazi kubwa kuifufua
na kuiunda upya baada ya kusambaratika mwaka 1977.