Jeshi la Polisi mkoani Temeke,
linamshikilia dereva wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
aliyefahamika kwa jina la Bw. Samwel Mulagalazi, ambaye anadaiwa
kushirikiana na watu wawili waliotaka kumtapeli mteja wa Shirika la
Umeme nchini (TANESCO), sh. milioni 60.
Tukio hilo limetokea juzi saa 11 jioni
katika kiwanda kilichopo Mbagala, Dar es Salaam (jina tunalo), ambapo
matapeli (vishoka), waliojifanya wafanyakazi wa TANESCO, Makao Makuu,
Ubungo, walitaka kufanya utapeli huo kwa mmiliki wa kiwanda hicho.
Matapeli hao walimpigia simu mmiliki wa kiwanda hicho (jina tunalo), wakidai kiwanda chake kinaiba umeme hivyo walimtaka atoe sh. milioni 60 asiweze kukatiwa umeme.
Mmiliki huyo akitambua kuwa mita zake
hazikuwa na tatizo lolote na hahusiki na wizi huo, aliwasiliana na
Meneja wa TANESCO wilayani Temeke, Mhandisi Richard Mallamia na
kumweleza vitisho alivyopewa na matapeli hao na pesa waliyotaka kupewa.