Valence Robert, Geita
KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi
(15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kuonekana
akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya mwili wake
kukutwa ndani.
Kazi hiyo
iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi
ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua
taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya
jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati
ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina
lake mara moja naye akianguka na kuzirai.
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza
na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua
kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya
vipimo.
"Lengo la
kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha mwili wa
marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu
anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye," alisema.