Baadhi ya wachambuzi na wachunguzi wa
masuala ya kiusalama na kimataifa, wameyataja mambo matatu ambayo
yanathibitisha pasipo shaka kwamba waliotekeleza tukio hilo la kuvamia,
kuteka nyara na kuua watu wapatao 68 katika Kituo cha Biashara cha
Westgate, ni wa aina ya kundi ambalo kinadharia na kimatendo linafanana
na lile la kigaidi duniani la Al-Qaeda. Mambo yanayotajwa na wachambuzi
na wachunguzi hao ni pamoja na mbinu, teknolojia na aina ya watu
waliotumika kutekeleza shambulio hilo.
Katika uchambuzi wao, wameeleza kuwa
mbinu iliyotumiwa na magaidi hayo kuvamia pasipo kujulikana mara moja na
vyombo vya ulinzi na usalama vya nchini Kenya, lakini pia aina ya
silaha walizokuwa nazo, inaonyesha kuwa kundi hilo limeamua kutumia
kivuli cha Al-Shabab kufikisha ujumbe kwa dunia kwamba lipo licha ya
uongozi wake kubadilika.
Kwamba mbali na mbinu pamoja na
teknolojia, pia aina ya watu waliohusika kutekeleza shambulio hilo ambao
wamebainika kutoka katika mataifa mbalimbali duniani, ndio ambao
wamewafanya wachambuzi na wachunguzi hao waanze kupata shaka kwamba
huenda kuna kundi kubwa zaidi lililotekeleza shambulio hilo, ambalo
limejivika taswira ya Al-Shabab.